Home Mchanganyiko JAFO AFURAHISHWA UJENZI MIRADI YA KIMKAKATI HALMASHAURI YA MJI NJOMBE, WAKANDARASI...

JAFO AFURAHISHWA UJENZI MIRADI YA KIMKAKATI HALMASHAURI YA MJI NJOMBE, WAKANDARASI WALIA NA MSAMAHA WA VAT.

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe Salum Hamdun,Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Wataalamu Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Mji Njombe  wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la kisasa katika Halmashauri Ya Mji Njombe
Mhandisi anayesimamia ujenzi wa soko la kisasa Njombe Justin Mboka akiwa ameambatana na Waziri Jafo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa soko la kisasa katika Halmashauri ya Mji Njombe
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo akitoa maelekezo wakati alipokagua shughuli za uendeshaji stendi mpya Njombe.
Ujenzi wa soko la Kisasa ukiendela katika Mtaa wa Kwivaha Halmashauri ya Mji Njombe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo akiwa anazungumza na wasafiri na wadau wa usafirishaji waliokuwepo katika stendi kuu mpya Njombe
Mratibu wa Mradi wa ujenzi wa stendi Mhandisi Damasco Tembo wa (kwanza kushoto) akitoa maelezo ya shughuli zilizosalia za ujenzi wa stendi mpya ya mabasi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo wakati alipokagua stendi hiyo.Kulia kwa Jafo ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri akifuatiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri Illuminatha Mwenda
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo akizungumza na Mama Lishe(hawapo pichani ) wanaofanya biashara zao katika eneo la stendi mpya ya Njombe
Mhandisi anayesimamia ujenzi wa soko la kisasa Njombe Justin Mboka akimuonesha Waziri Jafo matenki yaliyochimbwa ardhini kwa ajili ya kuifadhi maji yatakayovunwa katika eneo la soko.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya stendi na ujenzi wa soko.Nyuma ya Mkurugenzi ni Mwenyekiti wa Halmashauri Edwin Mwanzinga

******************************************

Hyasinta Kissima- Afisa Habari H/Mji Njombe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Selemani Jafo ameonyesha kufurahishwa na ujenzi wa soko la kisasa katika Halmashauri ya Mji Njombe ujenzi ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo octoba 2019 na kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.9.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kuona shughuli za ujenzi zinazoendelea katika soko hilo Jafo amesema kuwa licha ya kuwepo na ujenzi wa miradi ya masoko katika Mikoa ya Mtwara, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam ujenzi wa soko la Njombe ni wa kipekee na wenye viwango vya hali ya juu na kufurahishwa na namna Halmashauri ilivyoweza kuwashirikisha wafanyabiashara katika kila hatua za ujenzi na kutoa ushauri wao na kwa jinsi Halmashauri ilivyoweza kubuni na kutenga eneo kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua ambayo
yatakuwa yakihudumia eneo lote la soko jambo ambalo limekuwa halitekelezwi kwenye miradi mingi.

“Mimi huwa nakuja kukagua kazi sio kutembelea. Binafsi nimeridhishwa na kufurahishwa sana na ujenzi unaoendelea wa soko. Hiki ni kitega uchumi kikubwa sana kwa Halmashauri na kitabadili mandhari ya Mji wa Njombe. Katika Kanda ya Nyanda za juu kusini soko hili litakuwa la kipekee niwapongeze mmefanya kazi nzuri na hamjanitia hasira. Mkandarasi unafanya kazi nzuri sana na ninaomba uhakikishe kuwa unamaliza kazi kwa wakati.”Alisema Jafo.

Awali akipokea taarifa ya maendeleo ya shughuli za uendeshaji wa stendi na umaliziaji wa ujenzi kutoka kwa Mratibu wa Mradi Mhandisi Damasco Tembo, Mhandisi huyo alisema kuwa kwa sasa ujenzi wa stendi hiyo umekamilika kwa asilimia 96 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni 2019 na kubainisha changamoto kubwa ya kutopatiwa kwa msamaha wa ongezeko la thamani VAT kwa Wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi wa soko na stendi jambo linakwamisha kukamilika kwa wakati kwa miradi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa hiyo Jafo ameahidi kushughulikia changamoto ya msamaha wa ongezeko la thamani VAT changamoto iliyoibuliwa na wakandarasi wote wanaotekeleza ujenzi wa mradi wa soko na stendi na ameitaka Halmashauri kupata suluhu ya jambo lililokwamisha uwepo wa ujenzi wa kituo cha mafuta ndani ya stendi kama ilivyokuwa kwenye mchoro wa awali.

“Lengo la miradi hii ni kwa ajili ya kukuza Miji na kuzijengea Halmashauri uwezo wa kujitegemea. Kama ramani ya stendi hii ilikua na eneo la kituo cha mafuta, na eneo limetengwa rasmi kwa ajili ya shughuli hiyo sioni sababu ya kusitisha ujenzi wa kituo hicho. Kama ni sababu za kiusalama zilizowafanya kusitisha ujenzi wa kituo hicho cha mafuta sina shaka nalo lakini kama mmesitisha kutokana na ushauri kwamba maeneo ya jirani na stendi kuna kituo cha mafuta basi Miji mingine isingekuwa na vituo vya mafuta maana kila sehemu vipo mimi nadhani hiyo ya kuwepo kwa vituo vya jirani sio hoja.’’Jafo alifafanua
Jafo aliendelea kusema “Swala la msamaha wa VAT ni changamoto inayoikabili miradi mingi inayosimamiwa na TAMISEMI. Hapa Njombe naona tena changamoto hii inajirudia licha ya Mheshimiwa Rais kutoa maelekezo kuhusiana na suala hili. Naomba nichukue changamoto hii na nitaiwasilisha kwa Waziri wa Fedha kwa utekelezaji. Mimi nataka Halmashauri hizi zifuzu na kufikia uchumi wa kujitegemea.”Alisema

Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri amemuahidi Mheshimiwa Jafo kuendelea kusimamia kwa ushirikiano shughuli zilizosalia za ujenzi na kumwambia kuwa pale patakapohitaji msaada hawatasita kuwasiliana kwa ajili ya kuhakikisha kuwa changamoto zinatatuliwa ili Wananchi wa Njombe waweze kunufaika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amemshukuru Mheshimiwa Jafo kwa kutembelea mradi wa soko na kukagua shughuli za uendeshaji wa stendi na kuahidi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri huyo katika ziara yake.

“Sisi tutaendelea kusimamia kazi hizi kwa nguvu zote. Tutakuwa na vikao kila wiki kuangalia hatua ya namna gani tunamaliza shughuli za soko. Kuhusu wazo la kuendelea na ujenzi wa kituo cha mabasi ndani ya stendi tutaangalia sheria, kanuni, taratibu na hali za kiusalama kama vyote vinaruhusu tuone namna ya kurejesha ule mradi katika stendi yetu mpya.”Alisema Mwenda.

Mradi wa ujenzi wa stendi unatarajiwa kuingizia Halmashauri mapato ya zaidi ya milioni mia mbili hamsini kwa mwaka huku mradi wa soko ukitarajiwa kuingiza zaidi ya milioni mia tatu kwa mwaka pindi itakapokamilika.