Wanafunzi wa Shule ya sekondari ya Mnyakongo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma wakipokea mabati – muda mfupi kabla ya Benki ya NMB kukabidhi msaada huo wa Mabati 250 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya shule hiyo.
Spika wa Bunge Job Ndugai akikata utepe kama ishara ya kupokea msaada wa Mabati 250 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya shule ya sekondari Chiwe na meza na viti 126 kwa ajili ya shule ya sekondari Mnyakongo zote za Wilayani Kongwa. Msaada huo una thamani ya shilingi Milioni 10. Wengine katika Picha ni Mjumbe wa Bodi ya NMB – Margaret Ikongo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa – Zuberi White (kulia kwake), kushoto ni Afisa Mkuu Uendeshaji, Bidhaa na Matumizi ya Digitali wa NMB – Pete Novat na Meneja wa NMB Kanda ya Kati Nsolo Mlozi
Spika wa Bunge Job Ndugai akimshukuru Mjumbe wa Bodi ya NMB – Margaret Ikongo mara baada ya kupokea msaada wa Mabati 250 kwa ajili ya ujenzi wa maabala ya shule ya sekondari Chiwe na Meza na Viti 126 kwaajili ya shule ya sekondari Mnyakongo zote za Wilayani Kongwa. Msaada huo una thamani ya shilingi Milioni 10. Makabidhiano hayo yalifanyika jana shuleni Mnyakongo.
Wanafunzi wa Shule ya sekondari ya Mnyakongo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma wakifurahia viti na meza walivyokabidhiwa na Benki ya NMB ili kukabili uhaba wa madawati
…………………………………………….
SPIKA wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai ameiomba Benki ya NMB kutoa elimu kwa wananchi ili wajue jinsi ya kutunza fedha za mikopo yao.
Ndugai ameyasema hayo wakati wa NMB ilipofanya ziara ya kukabidhi viti na meza 63 vyote vikiwa na idadi hiyo kwa Shule ya Mnyakongo pamoja na mabati 250 kwa Shule ya Chiwe zilizopo Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Spika amesema kuwa NMB wanakila sababu ya kuendelea kutoa elimu ya utunzaji fedha kwa wananchi kama wanavyofanya kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari ili wawe na ujuzi zaidi.
Aidha amesema kuwa watu wengi wanakopa fedha lakini hawajui wafanyie nini baada ya kuzichukua.
‘’Yaani unashangaa muda mchache ukikutana na watu hao hakuna cha maana walichofanyia badala yake wanarudi katika maisha yya chini badala ya kusonga mbele kimaisha’’amesema Ndugai
Spika Ndugai amesema kutokana na hilo kuna sababu ya elimu hiyo kutolewa kwa wananchi ili wakope fedha huku wakijua wanakwenda kuzifanyia nini.
Ndugai amefafanua kuwa ameshakutana na kesi hizo nyingi kwa ndugu jamaa na marafiki ambao wamekopa bila ya kupata mafanikio yoyote.
‘’Kwa kweli kwa hilo naomba mlifanyie kazi kwani limekuwa likiwaumiza wananchi na kupelekea kurudi nyumba kimaendeleo badala ya kwenda mbele katika maisha kupitia fedha walizokopa’’amesisitiza Ndugai
Kwa upande wake Meneja wa NMB kanda ya kati Nsolo Mlozi amesema kuwa wataendelea kuiunga mkono Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli hivyo wametenga maeneo manne kwa ajili ya kusaidia jamii.
Mlozi ameyataja amaeneo hayo ni Elimu,Afya,Kilimo na utunzaji Fedha kwa vijana mpaka watu wa rika la juu kwa lengo la kuwainua kiuchumi kwa kunufaika kwa kupitia NMB.
Hata hivyo amesema kuwa mpaka sasa tayari milioni 400 zimeshatolewa kwa ajili ya misaada katika shule na hospitli ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa.Mlozi amesema kuwa NMB iko pamoja na serikali kuhakikisha wanafikia malengo waliojiwekea.
Naye Mkuu wa Shule ya Mnyakonga Mpokeeni Sanga amesema kuwa walikua na upungufu wa madawati 70 na wanaishukuru NMB kuwapa viti 63 na meza 63 na ambavyo wanaamini vitasaidia kupunguza uhaba waliokuwa nao.
Sanga amewahakikishia NMB kuwa vitu hivyo watavitunza ili hapo wanafunzi wengine waje kuvitumia hapo mbeleni na amewaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia jamii kwani wamekuwa mfano wa kuigwa nchini.
Mkuu wa shule ya Chiwe Aron Mango amesema kuwa mabati hayo waliopewa yatawasaidia kuezeka mabweni ya wasichana ambayo yanajengwa shuleni hapo