Aidha Jeshi hilo limesema jambo hilo ni udhalilishaji wa utu wa binadamu na kwamba suala la kutumia picha za vijana hao ambao hawahusiki katika habari hiyo ni cha ukosefu wa maadili ya uandishi wa habari .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 6,2023 jijini Dodoma Mkuu wa Tawi la utawala wa JKT ,Brigedia Jenerali Hassan Mabena,amevitaka vyombo vyote vya habari na mitandao ya kijamii vilivyoripoti habari hiyo kwa kuweka picha za vijana wa JKT ambao si wahusika wa habari hiyo kuomba radhi na kuondoa picha hiyo mara moja .
“JKT tumeumizwa na taswira hiyo kwa sababu vijana hao hawahusiani na habari hiyo, ufafanuzi ni kwamba mafunzo ya vijana wa kundi la lazima ambao ni wahitimu wa kidato cha sita huendeshwa Kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo kabla ya kuanza mafunzo hufanyiwa usahili wa nyaraka zao Pamoja na vipimo vya afya kufahamu utimamu wa mwili,”amesema
Pamoja na hayo Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana ambao majibu ya vipimo vyao kuwa na changamogo za kiafya hufanya mafunzo yao chini ya uangalizi wa wakufunzi ili kuhakikisha wanamaliza mafunzo salama bila msongo wa mawazo.
“Kwa kuwa hili ni kundi la lazima,vijana Wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho hupokelewa katika kikosi cha Ruvu JKT ambacho kina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo,”amesema na kuongeza;
JKT inasisitiza kuwa kigezo cha afya kwa vijana hao wa kundi la lazima wanaokuja makambini wakiwa na changamogo za kiafya kinazingatiwa kwa kuwaweka chini ya uangalizi na si vinginevyo.
“JKT tunazingatia sheria,kanuni na taratibu za kitabibu sambamba na kuzingatia Mila na desturi za nchi yetu Katika kutekeleza jukumu lake la msingi la malezi ya vijana,Umma unapaswa kufahamu kuwa mafunzo ya JKT ni salama na yenye kuzingatia miongozo ya malezi ya vijana,”amesisitiza
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,,amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa kufuata weledi wa taaluma zao wanaporipoti matukio mbalimbali.
“Sote tunafahamu kuwa Katika habari hii uhuru wa vyombo vya habari haukuzingatiwa, lazima wahusika waombe radhi ili kuwaweka salama vijana wetu,”amesisitiza Msigwa.