|
Kampuni ya Aspire Products & Services Co. Ltd (APS Company) inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa Taulo za kike maarufu kwa jina Kipepeo Pad imetoa msaada wa taulo za kike 400 kwa wanafunzi 30 wanaosoma katika shule ya msingi Ushirika na shule ya Sekondari Chamaguha zilizopo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga.
Hafla fupi ya makabidhiano ya Taulo za kike ‘Pedi’ imefanyika leo katika shule ya Ushirika na Chamaguha na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya APS Janeth Dutu aliyeambatana na baadhi ya waliokuwa wanafunzi wa shule ya msingi Ushirika ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko.
Akizungumza wakati wa kupokea Taulo hizo za kike kutoka Kampuni ya APS, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko aliishukuru Kampuni ya APS kwa msaada huo akibainisha kuwa zitasaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi wa kike wanapokuwa katika hedhi.
“Asanteni sana APS Company kwa msaada wa taulo za kike kwa ajili ya wanafunzi 10 wanaosoma katika shule ya msingi Ushirika na wanafunzi 20 wanaosoma katika shule ya sekondari Chamaguha watakazozitumia kwa muda wa mwaka mmoja. Hakika mmeunga mkono kwa vitendo kampeni yetu ya ‘Msitiri msichana,punguza utoro shuleni’ tuliyoianzisha hivi karibuni”,amesema Mboneko.
“Tunakushukuru ndugu yetu Janeth Dutu kupitia Kampuni yako ya APS pamoja na waliowahi kuwa wanafunzi wa shule ya msingi Ushirika ambao umeambatana nao leo kuleta taulo za kike. Hii ni sadaka kubwa mmetoa”,ameongeza Mboneko.
Mkuu huyo wa wilaya ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia upatikanaji wa taulo za kike shuleni kwani bado wanafunzi wa kike wanapata changamoto akieleza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira rafiki.
Katika hatua nyingine Mboneko amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kuepuka vikundi viovu na vishawishi mbalimbali vinavyoweza kukatisha ndoto zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aspire Products & Services Co. Ltd (APS), Janeth Dutu amesema lengo la kutoa taulo za kike ni kupunguza utoro shuleni kwani baadhi ya wanafunzi wa kike wamekuwa hawaendi shuleni kutokana na kukosa taulo za kike wanapokuwa katika hedhi.
Amesema kutokana na uwepo wa taulo za kike wanafunzi watahudhuria masomo yao hata kama wapo katika hedhi hivyo ufaulu wao utaongezeka.
“Ninaamini kabisa taulo zetu za kike zinazojulikana kwa jina la Kipepeo Pad ambazo zina ubora wa hali ya juu zitawasaidia wanafunzi 10 katika shule ya msingi Ushirika ambayo nilisoma lakini pia wanafunzi 20 katika shule ya sekondari Chamaguha ambapo nitaendelea kuwahudumia wanafunzi hawa kwa muda wa mwaka mmoja”,amesema Janeth.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi walionufaika na msaada huo, Elizabeth Kagongoo kutoka shule ya sekondari Chamaguha ameishukuru Kampuni ya APS kwa kuwapatia taulo za kike akieleza kuwa awali walikuwa wanalazimik kutumia vitambaa na wakati mwingine baadhi yao kuwa watoro shuleni pindi wanapokuwa katika hedhi.