WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amewataka wahitimu wa Taasisi ya Uongozi nchini kuzingatia zaidi maadili, nidhamu na ujasiri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza Mei 15, 2026 katika mahafali ya tisa ya taasisi hiyo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kikwete alisema uongozi bora wa sasa unahitaji watu wenye msimamo thabiti wa kimaadili, weledi na moyo wa uzalendo ili kuweza kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za umma na sekta binafsi.
Amesema katika mazingira ya sasa ya kiuchumi na kijamii, kiongozi anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa uaminifu na uwajibikaji, huku akisisitiza kuwa maarifa na ujuzi wanaopata wahitimu hao yanapaswa kutafsiriwa katika vitendo vinavyoleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Uongozi wa umma unahitaji watu waadilifu, wazalendo na wanaojitambua. Pale tunaposhindwa kulinda rasilimali za umma, tunakuwa tumepoteza imani ya wananchi. Ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka ni aina ya usaliti kwa taifa letu,” alisema Kikwete.
Aidha, aliwahimiza wahitimu hao kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika taasisi wanazozitumikia, wakilinda mali za umma na kuhakikisha kila hatua wanayochukua inalenga kuleta manufaa mapana kwa wananchi badala ya maslahi binafsi.
Amesema Tanzania inahitaji viongozi wenye maono, uwazi, uwajibikaji na uadilifu, ambao wataweza kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuifanya nchi kuwa mfano bora barani Afrika katika masuala ya utawala bora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, alisema jumla ya wahitimu 231 wametunukiwa vyeti baada ya kukamilisha kwa mafanikio programu mbalimbali za uongozi zinazotolewa na taasisi hiyo.
Singo isema Kozi zote zinalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kiuongozi, usimamizi, maamuzi bora na mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali katika taasisi na jamii.
Aliongeza kuwa wahitimu hao wameonesha mabadiliko makubwa katika utendaji kazi wao, kujiamini na uwezo wa kufanya maamuzi yenye tija, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa mafunzo hayo katika kuimarisha uongozi bora nchini Tanzania.

