
Uongozi wa Taasisi ya LALJI FOUNDATION ukiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) mkoani Kigoma mara baada ya kukabidhi mizinga 50 ya nyuki, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wajane kiuchumi kupitia ufugaji nyuki.


………….
Katika juhudi za kuwawezesha wanawake wajane kujikwamua kiuchumi, Taasisi ya LALJI FOUNDATION imekabidhi mizinga 50 ya nyuki kwa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kukuza kipato kupitia ufugaji nyuki.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Katibu wa LALJI FOUNDATION, Bi. Fatema Imtiaz Lalji, amesema kuwa huo ni mwanzo wa utekelezaji wa mpango mkubwa unaolenga kugawa jumla ya mizinga 200 kwa wajane katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema taasisi hiyo imeanza na mkoa wa Kigoma kwa kuwalenga wajane, ambao mara nyingi hukumbana na changamoto za kiuchumi na kijamii, hivyo kuwapatia fursa ya kujipatia kipato kupitia ufugaji nyuki.
“Tunatambua mchango wa wanawake katika jamii, lakini pia tunatambua changamoto wanazokutana nazo, hususan wajane. Kupitia mradi huu, tunalenga kuwapa uwezo wa kujitegemea kiuchumi,” amesema Bi. Lalji.
Ameongeza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu, huku taasisi hiyo ikiendelea kufikia makundi mbalimbali yenye uhitaji katika maeneo tofauti nchini.
Amesema Kabla ya kukabidhi mizinga hiyo LAJI FOUNDATION iliendesha mafunzo ya kitaalamu kwa wanufaika wa mradi huo ambayo yalifanyika Febuari 15, 2026 Wilayani Bagamoyo ili kuhakikisha wanapata ujuzi sahihi wa utunzaji wa mizinga, uvunaji wa asali kwa njia salama, pamoja na uhifadhi wa bidhaa zitokanazo na nyuki.
“Mafunzo hayo yatasaidia kuongeza tija na ubora wa mazao, hivyo kuwawezesha wajane hao kushindana katika soko”
Ameongeza kuwa pamoja na kugawa mizinga, pia kuna mpango wa kuwasaidia wanufaika kupata masoko ya uhakika ya bidhaa zao, ikiwemo asali na nta, ili kuhakikisha wanapata faida stahiki. Hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto ya soko ambayo imekuwa ikiwakwamisha wafugaji wengi wadogo nchini.
Kwa upande wao, wanachama wa CCWWT mkoani Kigoma wameishukuru LALJI FOUNDATION kwa msaada huo, wakisema utasaidia kubadilisha maisha yao na kuongeza kipato cha familia.
Wamesema ufugaji nyuki ni fursa muhimu inayoweza kuleta maendeleo endapo watapatiwa elimu na usimamizi mzuri, huku wakiahidi kuitunza na kuitumia vizuri mizinga hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wajane hao, huku ukichangia pia katika uhifadhi wa mazingira na uzalishaji wa mazao ya nyuki kama asali, nta na bidhaa nyingine zitokanazo na nyuki.
