Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bi. Maryam Ahmed Muhaji amemuagiza Afisa elimu Mkoa wa Manyara kusimamia zoezi la kufungua Klabu za Maadili kila Shule na vyuo vilivyopo mkoani Manyara ili kuendeleza kukuza maadili mkoani humo.
Bi.Maryam ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya Maadili kwa walimu walezi wa Klabu za Maadili mkoani Manyara yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara tarehe 21 Aprili, 2026.
“Pamoja na kuwa jukumu la malezi ya maadili yanaanzia nyumbani lakini ni wazi kuwa waalimu ndio mna mchango mkubwa katika kukuza maadili ya wanafunzi kwa sasa kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na tamaduni zetu, waalimu ndio mnabaki na watoto muda mrefu, hivyo Serikali inawategemea sana kwa hili.” alisema Bi. Maryam.
Aidha Bi. Maryam ameongeza kuwa mwanafunzi anapoingia shuleni uyo ni mtoto wa mwalimu, hivyo ni lazima tuanze kukumbushana maadili bora na lazima tuwafundishe namna jamii inavyoishi kwani bila maadili ata ufaulu wa wanafunzi utashuka.
“Tumeshuhudia baadhi ya wanafunzi wanaaribikiwa shuleni wakati mzazi na mlezi wamejitahidi kumlea kwa weledi na hii ndio sababu inayopelekea sisi Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili kuanzisha Klabu za Maadili kwa kila shule,” alisema.
Kwa mujibu wa Katibu Tawala huyo wa mkoa wa Manyara, jukumu la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kusimamia na kukuza maadili tu, lakini wanaotengeneza maadili na kuweka msingi imara ni wazazi na walimu.
Aidha, Kiongozi huyo amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Manyara kuhakikisha wanazilea klabu za maadili kwa kuhakikisha wanatenga bajeti ya kuziendeleza klabu hizi kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili.
Kwa upanda wake Mwalimu, Kassim Jamal kutoka Sekondari ya Qash katika Halmashauri ya wilaya ya Babati amesema utekelezaji wa agizo la Katibu Tawala wa Mkoa utakwenda kuwa chachu ya kuongeza ufaulu mkoani Manyara kwa kuwa maadili ndio msingi wa mambo mazuri.
Naye Katibu Msaidizi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini, Bw. Gerald Mwaitebele amempongeza Katibu Tawala wa Mkoa huo kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha maadili yanakuwa bora mkoani humo na amehaidi kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itashirikiana na Halmashauri zote za mkoani huo kuhakikisha shule zinakuwa na Klabu za Maadili ambazo ni hai.




