Mwamvua Mwinyi- Mafia
April 22,2026
Jumla ya miradi saba yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.45 imepitiwa na Mwenge wa Uhuru wilayani Mafia, ikiwemo miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi.
Kati ya miradi hiyo, miwili imekaguliwa, mitatu imezinduliwa na miwili imewekewa mawe ya msingi, huku Mwenge ukikimbizwa kwa umbali wa kilomita 79.1 katika wilaya hiyo.
Mwenge wa Uhuru umewasili wilayani Mafia Aprili 22, 2026 ukitokea wilayani Kibaha, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, ameukabidhi rasmi kwa Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Mwango’nda, ameridhishwa na usimamizi na utekelezaji wa miradi hiyo, akiwataka viongozi wa wilaya, halmashauri na taasisi mbalimbali kuhakikisha wanawahusisha wananchi kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, amewapongeza wananchi waliojitolea kutoa maeneo yao kwa ajili ya miradi ya Serikali, akisema hatua hiyo inachangia maendeleo ya vijiji, wilaya na Taifa kwa ujumla.
Mwang’onda amewasihi wananchi kuitunza miradi hiyo ili iweze kudumu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 zinaongozwa na kaulimbiu isemayo:
“Tanzania ni Yetu Sote, Tushirikiane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”





