* Baraza la Madiwani kupitia upya tozo kandamizi kwa Wakulima.
Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Karagwe kuwa ataendelea kushirikiana kwa ukaribu na Madiwani katika kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na kutatua changamoto na mahitaji ya wananchi ambapo ameeleza kuwa kipindi hiki kinampa nafasi na muda mpana zaidi wa kuwatumikia kwa ufanisi kama mwakilishi wao ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameitoa kauli hiyo leo, tarehe 2 Desemba 2025, katika kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, kikao kilichohusisha viapo vya madiwani pamoja na uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.
Bashungwa amesema kuwa katika kipindi hiki ameendelea kuboresha Ofisi ya Mbunge ili kuwasogelea na kuwahudumia wananchi kwa ukaribu zaidi ambapo atafungua ofisi mbili ndogo za Mbunge katika maeneo ya Rwambaizi na Nyaishozi, na tayari amenunua magari mawili aina ya “pickup” kwa ajili ya kuimarisha huduma kwa wananchi.
“Kipindi hiki ambacho nimepata muda wa ziada, niwahakikishie Wanakaragwe, kazi hii ya Ubunge niliiomba kutoka kwenu, mkaniamini na mnaendelea kuniamini. Nitatumia muda huu, hata kama ni kutembea kwa miguu au kwa njia yoyote ile, kufika kwenye vitongoji na vijiji vyote kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa amesema watashughulikia kero ya tozo kandamizi zinazowaumiza wakulima wanapopeleka mazao yao kwenye masoko na magulio kwa kushirikiana na Madiwani kuhakikisha zinapitiwa upya na kufanyiwa maboresho, sambamba na kuisimamia Halmashauri kufanya marekebisho ya kanuni ili kuondoa vikwazo vinavyowanyima wananchi tija na ustawi katika shughuli zao.
Aidha, Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani aliyomwonyesha katika kipindi kilichopita kwa kumpatia majukumu mbalimbali ya kuwatumikia Watanzania katika Serikali ya Awamu ya Sita.
Pia, amewashukuru wananchi wa Wilaya ya Karagwe kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge pamoja na Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Akizungumzia miradi ya maendeleo, Bashungwa amesema ataendelea kushirikiana na Madiwani kusimamia kikamilifu miradi inayoendelea na ile mipya itakayoanza kutekelezwa katika Wilaya ya Karagwe, ikiwemo ujenzi wa Soko la Kisasa Kayanga na ujenzi wa stendi mpya ya Kishao.
Katika hatua nyingine, Bashungwa amewapongeza Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Longino W. Rwenduru (Diwani wa Kata ya Chanika), pamoja na Makamu Mwenyekiti, Adriani R. Kobushoke (Diwani wa Kata ya Rugu), kwa kuchaguliwa kwa asilimia mia moja kuongoza Baraza la Madiwani.




