Na Ofisi ya Mkuu Wa Mkoa wa Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule,amewatembelea wanafunzi wa shule ya sekondari Mtera Dam katika Wilaya ya Mpwapwa na kuwapa pole kufuatia madhila ya kuunguliwa na Bweni hapo Novemba 12, 2025 na kupoteza kila kitu hali iliyoulazimu uongozi wa Wilaya hiyo kufanya utaratibu wa kuwahamishia kwenye shule mbili za Mazae na Kimaghai ili waweze kuendelea na masomo.
Mhe. Senyamule alifika shule moja wapo ya Mazae Novemba 13, 2025 akiwa ameambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dkt. Khatibu Kazungu, Kamati ya Usalama Mkoa na Afisa Elimu Mkoa ambapo wametoa baadhi ya mahitaji muhimu yatakayowawezesha wanafunzi hao wa kike kuweza kuendelea na masomo yao pasi na changamoto yeyote.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mhe. Senyamule amesema jambo jema la kumshukuru Mungu ni kwamba hakuna maisha ya mwanafunzi yeyote yaliyopotea zaidi ya vitu tu ambavyo vinaweza kutafuta ila uhai wa mtu hauwezi kutafutwa.
“Katika ajali hiyo mbaya ambayo mliunguliwa kila kitu, lipo jambo moja la kumshukuru Mungu kwa sababu kati yetu hakuna aliyeungua wala kupata madhara zaidi ya kuunguliwa na vitu, vitu vinatafutwa, watu hawatafutwi”.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huyo ameupongeza uongozi wa Wilaya kwa jitihada za kuhakikisha wanafunzi hao ambao ni kidato cha tano na sita wanaendelea na masomo kama kawaida kwa kuwa lengo kubwa ni kupata elimu lakini mahitaji mengine ni ya ziada.
“Huku mmekuja kutafuta Elimu, mmekuja kusoma, hapa Mazae kuna shule kama yenu, Ina masomo kama ya kwenu, ndio maana mkaletwa Mazae sekondari, katika hali ya kawaida mngeweza kuambiwa rudini nyumbani mkakae mwezi mmoja mpaka tujipange lakini wakasema hapana, hawa watoto ni Kidato cha tano na sita wanatakiwa kusoma kwa bidii ili kidato cha sita wajiandae na mitihani mwaka kesho”. Mhe. Senyamule.
Hata hivyo kwa Mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Dkt. Sophia Kizigo, uchunguzi wa awali unaonesha ajali hiyo imesababishwa na hitilafu ya umeme kutokana na uchakavu wa miundombinu ya nishati hiyo ndani ya jengo hilo la Bweni hivyo Wilaya ina jukumu la kupitia upya na kurekebisha miundombinu hiyo kwenye Majengo mengine shuleni hapo ili kuepusha kutokea tena kwa kadhia hiyo.
Baadhi ya mahitaji aliyopeleka kwa wanafunzi hao wa kike wapatao 141 yatakayowawezesha kuendelea na masomo yao pasi na bughudha ni mabegi ya shule, ndoo za kuogea, miswaki, dawa za meno, sabuni, mafuta ya kujipaka, taulo za kike na mahitaji mengine ambayo yatakua faraja kwa wanafunzi hao.



