Mahenge, Morogoro
Katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia Mwaka 2022 hadi 2025 zimetolewa leseni 714 katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge zikijumuhisha leseni za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini kwa wadau mbalimbali wanajishughulisha na uwekezaji katika Sekta ya Madini.
Hayo yalielezwa Novemba 12, 2025 na Afisa Madini Mkazi , Mkoa wa Kimadini Mahenge Jonas Mwano wakati akielezea kuhusu mafanikio yaliyopo.
Mwano alisema kuwa, mafanikio hayo miaka mitatu yamepelekea kufikia lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa asilimia 78.7 katika wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero. Aidha katika kipindi cha mwezi Julai mpaka Oktoba 2025 Ofisi imekusanya asilimia 61 ya lengo katika kipindi husika.
Akielezea kuhusu aina ya leseni zilitolewa Mwano alifafanua kuwa, katika kipindi husika kulitolewa aina mbalimbali za leseni kama leseni za utafiti 15, leseni kubwa ya uchimbaji 2, leseni ndogo ya uchimbaji 277, leseni kubwa ya ununuzi 189 na leseni ndogo ya ununuzi madini 23.
Mwano aliongeza kuwa, Ofisi ya Madini Mkazi Mahenge inatoa leseni zinazompa haki mdau yeyote anaetaka kujihusisha na shughuli za madini kama vile uchimbaji , uongezaji thamani na biashara ya madini kama Sheria ya Madini Sura 123 inavyoelekeza.
Kuhusu mwenendo wa makusanyo wa maduhuli ya Serikali kwenye shughuli za mnyororo wa thamani madini, Mwano alisema kuwa, katika kipindi hicho Ofisi imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 2.8 sawa na asilimia 78.7 ya lengo iliyopangiwa.
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge pia imefanikiwa katika vipengele mbalimbali vinavyohusiana na shughuli za madini kama vile kuwajengea uelewa wachimbaji hususan katika masuala yanayohusu Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni zake, Utunzaji wa mazingira katika uchimbaji pamoja na kutoa elimu kuhusu masuala ya afya na usalama mahala Pa kazi.
Vile vile Ofisi imefanikiwa kupata jengo kubwa la soko la madini linalokidhi vigezo vya soko kulingana na idadi ya wafanyabiashara waliopo.
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mahenge ilianzishwa kwa mujibu wa mabadiliko ya Sheria ya Madini Sura ya 123 na kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi mwaka 2022.



