Na John Bukuku – Dar es Salaam
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi huduma mpya ya intaneti ya kasi inayojulikana kama T-Fiber Triple Hub Internet au Faiba Tipo Hub, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya shirika hilo kuboresha mawasiliano ya kidijitali nchini.
Akizungumza Novemba 12, 2025 wakati wa uzinduzi huo, Meneja Biashara na Promosheni wa TTCL, Janeth Maeda, alisema kuwa huduma hiyo mpya inaashiria hatua nyingine muhimu katika safari ya TTCL ya kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa Watanzania.
Amesema dunia kwa sasa inaendeshwa kwa nguvu za teknolojia na mawasiliano, hivyo huduma ya intaneti ya kasi siyo tena anasa bali ni hitaji muhimu katika maisha ya kila siku ya wananchi nyumbani, shuleni, ofisini na kwenye biashara.
Aidha, Maeda amebainisha kuwa TTCL imewekeza kikamilifu katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa urahisi, ubora wa juu na kwa gharama nafuu, ili kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali wanapoishi au wanapofanya kazi.
Amesema huduma hiyo mpya ya Faiba Tipo Hub imebuniwa mahsusi kwa kizazi cha kidijitali cha sasa, kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wanaotaka huduma bora, za uhakika na zinazotolewa kwa gharama nafuu.
Maeda ameeleza kuwa kifurushi hicho kimoja kinamuwezesha mteja kupata huduma ya intaneti ya kasi, simu ya mezani kupitia miundombinu ya faiba, pamoja na huduma ya simu ya mkononi yenye GB na dakika za kutosha kutumika popote pale mteja alipo.
Amesema huduma hiyo ni suluhisho kamili kwa familia, ofisi na biashara, kwa kuwa inarahisisha maisha, inapunguza gharama na inatoa thamani kubwa zaidi kwa wateja.
Aidha, amebainisha kuwa TTCL inalenga kuhakikisha kila nyumba, kila ofisi na kila mfanyabiashara nchini anakuwa sehemu ya mageuzi ya kidijitali, sambamba na kuunga mkono ajenda ya serikali ya kukuza uchumi wa kidijitali kupitia matumizi ya TEHAMA.




