Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani, ACP Joseph Mwakabonga (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Ltd, ambayo ni moja ya kampuni zilizo chini ya Oryx Energies, Bw. Benoit Araman, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania, Bw. Imani Mtafya, Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa, Bw. Said Chega, wakikata utepe ikiwa ni ishara uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa usalama barabarani ijulikanayo kama “Chuma kwa Chuma Sio Poa”, yenye lengo la kuwahamasisha Maafisa Wasafirishaji (Bodaboda) na bajaji kuzingatia sheria za usalama barabarani. Tukio hilo limefanyika leo Julia 19, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani, ACP Joseph Mwakabonga akizungumza na waandishi habari kuhusu umuhimu wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa usalama barabarani ijulikanayo kama “Chuma kwa Chuma Sio Poa”
Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Ltd, ambayo ni moja ya kampuni zilizo chini ya Oryx Energies, Bw. Benoit Araman akizungumzia umuhimu wa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa usalama barabarani ijulikanayo kama “Chuma kwa Chuma Sio Poa”
Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania, Bw. Imani Mtafya (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na dereva wa Pikipiki (Bodaboda) baada ya kumkabidhi vilainishi bora kwa mitambo ya pikipiki na magari.
Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa, Bw. Said Chega akieleza faida za kampeni hiyo.
…………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Kampuni ya Oryx Energies Tanzania Limited imezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa usalama barabarani ijulikanayo kama “Chuma kwa Chuma Sio Poa”, yenye lengo la kuwahamasisha Maafisa Wasafirishaji (Bodaboda) na bajaji kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Uzinduzi huo pia umeambatana na kukabidhiwa kwa vibanda vya kisasa kwa ajili ya askari wa usalama barabarani ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi wakiwa barabarani.
Akizungumza leo, Julai 19, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura, Kamishna Msaidizi wa Polisi kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani, ACP Joseph Mwakabonga, amesema kuwa kampeni hiyo itasaidia kuwajengea uelewa zaidi madereva wa Pikipiki (bodaboda) na bajaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
“Kampeni hii ya Oryx Energies imatoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda ni jambo mtambuka ambalo kila Mtanzania anatakiwa kuwa sehemu ya mafanikio yake. Tunawapongeza kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu hii kwa ndugu zetu wa bodaboda na bajaji,” amesema ACP Mwakabonga.
Amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwawezesha waendesha pikipiki na bajaji kuachana na tabia ya kutofuata sheria, jambo ambalo litasaidia kupunguza au kumaliza kabisa ajali zinazotokana na matumizi ya vyombo hivyo vya usafiri.
Aidha, Mwakabonga amebainisha kuwa ajali za barabarani bado ni changamoto kubwa nchini, hivyo ushiriki wa wadau kama Oryx Energies katika kutoa elimu ya usalama barabarani ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono.
Kuhusu vibanda vya kisasa vilivyokabidhiwa na kampuni hiyo, amesema vitasaidia askari wa kikosi cha usalama barabarani kutekeleza majukumu yao vizuri, kwani vimefungwa mfumo wa taa zinazotumia nishati ya jua (solar), hivyo kuwawezesha kufanya kazi hata wakati wa giza.
“Askari polisi sasa wanaweza kutekeleza majukumu yao wakati, kwani vibanda hivi vina taa zinazotumia nishati ya jua. Hii inaongeza ufanisi wa kazi zetu hata nyakati za usiku,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Ltd, ambayo ni moja ya kampuni zilizo chini ya Oryx Energies, Bw. Benoit Araman, amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuelimisha na kuhamasisha usalama barabarani, hasa kwa waendeshaji wa pikipiki na bajaji ambao ni sehemu muhimu ya usafiri wa kila siku.
“Tunaamini kwamba kwa pamoja tunaweza kupunguza ajali, kulinda maisha, kutumia nishati safi na kusaidia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa letu,” amesema Bw. Araman.
Amebainisha kuwa Oryx Energies pia imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania, Bw. Imani Mtafya, amesema kuwa kampeni hiyo imelenga kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya kwa waendesha pikipiki, bajaji na watoa huduma wengine kuhusu usalama barabarani.
Ameeleza kuwa malengo ya kampeni ya “Chuma kwa Chuma Sio Poa” ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendeshaji wa Pikipiki na bajaji kupitia ushirikiano na Jeshi la Polisi; pamoja na kutoa michango ya vitendea kazi kama vile vibanda vya kisasa vya askari vinavyotumia nishati ya jua, kofia ngumu, jaketi za kuonekana usiku, vizimia moto na vilainishi bora kwa mitambo, pikipiki na magari.
Aidha, kupitia kampeni hiyo, kampuni hiyo imetoa mafunzo ya usalama kwa wasafirishaji zaidi ya 200 kwa kila Wilaya Mkoa Dar es Salaam, huku ikilenga kutoa mafunzo mikoa yote.
Bw. Mtafya ametoa mwito kwa wasafirishaji na watumiaji wa pikipiki kuchangamkia fursa ya mafunzo na kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika jamii zao.
“Ajali nyingi zinaweza kuzuilika, elimu na uwajibikaji ni silaha kubwa zaidi,” amesisitiza Bw. Mtafya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa, Bw. Said Chega, amesema kuwa ni muhimu kuendelea kupatiwa elimu ya usalama barabarani.
Bw. Chega amesema kuwa kupitia kampeni ya “Chuma kwa Chuma Sio Poa”, ajali za barabarani zitapungua kwani waendesha bodaboda watakumbushwa mara kwa mara kuhusu kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Ameongeza kuwa kuna haja ya waendesha pikipiki kuendelea kupatiwa elimu kwa sababu wao husafirisha abiria kila siku, na hivyo wakipata elimu hiyo abiria wanakuwa salama.
“Tunawapongeza Oryx Energies kwa kampeni hii, lakini pia tunalishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwa mstari wa mbele katika kutupatia mafunzo haya mara kwa mara,” amesema Bw. Chega.