Mwenyekiti wa Watendaji Wakuu wa Mahakama kutoka nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika,Profesa Elisante Ole Gabriel,akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha leo.
Julieth Laizer, Arusha.
Arusha.Watendaji Wakuu wa Mahakama kutoka nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika,wanakutana Oktoba 22,mwaka huu jijini Arusha kujadili masuala mbalimbali ya uboreshaji wa huduma za mahakama ili ziweze kuwa msaada kwa wananchi kwa kutoa huduma bora na kusimamia utawala wa sheria.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mwenyekiti wa watendaji wakuu wa Mahakama wa nchi hizo,Profesa Elisante Ole Gabriel,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo.
Aidha mkutano huo unafanyika siku moja kabla ya Majaji wakuu 16 wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (SEACJF),kukutana jijini Arusha .
Ole Gabriel ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, amesema katika kikao hicho pamoja na mambo mengine watajadili na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za mahakama kwa wananchi ili kupunguza changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo.
Ametaja madhumuni mengine ya kikao hicho ni kujadilia masuala yanayohusu usimamizi wa mahakama,kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo na kuboresha ukuaji wao wa kitaaluma.
Aidha amesema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika ambapo Watendaji Wakuu wa Mahakama kutoka nchi hizo watapata nafasi ya kujadili na kuja na mpango wa kuleta mabadiliko.
“Tunatarajia kukutana na kufanya kikao Oktoba 22,2023 kabla ya mkutano wa jukwaa la majaji wakuu wa nchi zetu na tutajadiliana masuala mengi ya kuhakikisha tunaboresha huduma na kubadilishana uzoefu ili kuhakikisha masuala ya sheria na utawala yanasimamiwa kikamilifu,”amesema Ole Gabriel.
Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani,Dk Paul Kihwelo,amesema katika kubadilishana uzoefu wa utatuzi wa changamoto mbalimbali ili kuboresha huduma ya utoaji wa haki kwa wananchi majaji hao watakutana kwa siku nne kuanzia Oktoba 23,2023.
Ametaja nchi wanazotoka majaji hao ni Angola, Botswana, Eswatin, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zanzibar, Uganda, Zambia na Zimbabwe.