Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza Mrakibu Kamila Labani akielezea namna walivyoanza kuchukua tahadhari na hatua mbalimbali kwaajili ya kukabiliana na mvua za El- Nino.
Mrakibu Kamila Labani akiwa ameshika Raba Boti ambazo zinajazwa upepo na zikishajazwa zinaweza kutumika kufanya uokoaji kwenye madimbwi na maeneo yanayokuwa na maji ya muda mfupi.
…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza.
Kufuatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa (TMA) kuhusina na uwepo wa mvua za EL nino ambazo zinaweza kusababisha maafa makubwa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Mwanza limeanza kuchukua tahadhari na hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alihamis Oktoba 19, 2023 Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Mwanza Mrakibu Kamila Labani amesema, hatua ya kwanza walioanza nayo ni kuyatambua maeneo yote ambayo yanauwezekano wa kuwa kwenye hatari pindi mvua hizo zitakapoanza kunyesha.
“Tumetembelea Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza na tumeshabaini maeneo ambayo yako kwenye hatari,kwa Wilaya ya Nyamagana ni Mabatini,daraja la masai,Mkuyuni, pamoja na Nyashishi darajani maeneo haya yanakisiwa kuwa na changamoto ya kuwa na maji mengi yanayopita kwenye madaraja hivyo mvua zitakapoanza tunawashauri wananchi kuchukua tahadhari wakati wa kuvuka ili kuepusha madhara mbalimbali yanayoweza kujitokeza” amesema Mrakibu Labani.
Amesema mvua zitakapokuwa zimeaanza na kuonekana ni kubwa Jeshi hilo litapeleka askari kwenye madaraja ili waweze kufunga kodoni tepu kwaajili ya kuwasaidia wananchi wasivuke kwenye maeneo hatarishi.
Aidha, amewaomba wananchi wanaokaa kwenye mabonde kuanza kuchukua tahadhari mapema ikiwemo ya kuhamia kwenye maeneo ambayo yako juu ili kuepukana na maporomoko ya maji Yanayoweza kuleta madhara.
Mrakibu Labani ameeleza kuwa vifaa kwaajili ya uokoaji vipo zikiwemo Raba Boti ambazo zinajazwa upepo na zikishajazwa zinaweza kutumika eneo lolote kwaajili ya kufanya uokoaji kwenye madimbwi, na maeneo yanayokuwa na maji kwa muda mfupi pamoja na Faiba ambazo zinarekebishwa kwaajili ya kupamabana na changamoto hiyo itakapotokea.