Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Fatma Mrisho akimshauri Jambo Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maradhi yasioambukiza ambayo huanzia septemba 14 hadi 21 Kila mwaka Duniani kote , hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Unguja .
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh Akizungumza na Waandishi wa Habari katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maradhi yasioambukiza ambayo huanzia septemba 14 hadi 21 Kila mwaka Duniani kote, hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Unguja .
Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Mnazimmoja Dkt.Amour Sleiman Mohammed akichangia katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maradhi yasioambukiza ambayo huanzia septemba 14 hadi 21 Kila mwaka Duniani kote, hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Unguja .
……….
Na Fauzia Mussa, Maelezo
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh amewataka Wananchi kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa Afya kuhusu kujilinda na magonjwa yasioambukiza ili kushinda vita dhidi ya magomjwa hayo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika kilele cha wiki ya magonjwa yasioambukiza Naibu Hassan alisema kufanya hivyo kutapunguza wimbi la wagonjwa wa maradhi hayo wanaoongezeka siku hadi siku duniani kote .
Alisema kwa upande wa Zanzibar magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku na kusababisha vifo ,ulemavu pamoja na kuongeza utegemezi wa wagonjwa kwa familia kutokana na kuuguwa kwa muda mrefu.
“Wahenga walisema kinga ni bora kuliko tiba ,tuna kila sababu ya kujikinga na maradhi yasioambukiza hasa ukizingatia maradhi haya yanaweza kukingwa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya” Alisistiza Naibu huyo.
Alisema katika kuadhimisha wiki hiyo Wizara kupitia kitengo cha maradhi yasioambukiza kwa kushirikiana na Taasisi ya Pham Acces iliendesha zoezi la upimaji wa Afya kwa Wananchi wa Unguja na Pemba ambapo Takwimu zilithibitisha hali halisi ya Magonjwa hayo visiwani.
Alifahamisha kuwa kati ya watu 747 waliochunguzwa, watu 19 sawa 2.5% waligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha sukari, Watu 84 sawa na 11.2% waligundulika kuwa na shindikizo la juu la damu (Presha) na watu 124 sawa na 16.6% walionekana kuwa na uzito uliopindukia, hivyo alisema ipo haja ya kushirikiana na kuongeza juhudi katika kupambana na Magonjwa hayo ili kuyatokomeza nchini
Sambamba na hayo aliwataka wananchi kubadilisha mfumo wa chakula kwa kujitahidi kula mlo kamili unaofaa, kufanya mazowezi, pamoja na kuachana na vichocheo vyote vya maradhi yasioambukiza ili kuwa na Taifa lenye wananchi wenye Afya bora.
“tunajua kuwa katika jamii kubwa kama hatujala chipsi haturidhiki,tena inaliwa usiku halafu tunalala, tujue tunashibisha tumbo lakini tunakaribisha maradhi mengi ikiwemo yasioambukiza”alikumbusha Naibu huyo.
Nae Mwakilishi wa Taasisi ya PharmAcces Queen – Ruth Msina ameishukuru Serikali kwa kuthamini na kujali mchango wao wanaoutoa katika kupambana na vita dhidi ya magonjwa yasiambukiza.
Wiki ya Magonjwa yasioambukiza huanza Kila ifikapo septemba 14 na kufikia kilele chake septemba 21 Duniani kote ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Muda wa Kujali Kuhusu Maradhi Yasioambukiza”. PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR