WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa sh. milioni 500 za kujenga kituo kipya cha afya katika tarafa ya Nguruka, wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nguruka.
Waziri Mkuu amesema uamuzi huo unatokana na ombi la Mbunge wa Kigoma Kusini, Nashon Bindyaguze ambaye amekuwa akilalamikia udogo wa kituo kilichopo ikilinganishwa na idadi ya wakazi wa kata nne zilizopo.
“Mbunge wenu amekuwa akilalamikia udogo wa kituo cha afya kilichopo kwamba kinahudumia watu wengi kuliko uwezo wake. Nimeenda kukikagua, baadhi ya majengo yamechakaa, nimeelezwa zamani ilikuwa ni zahanati.”
Amesema kituo kipya cha afya kitakachojengwa kitakuwa na majengo ya kutolea huduma mbalimbali ikiwemo mapokezi, vyumba vya madaktari, maabara, vyumba vya upasuaji, jengo la mama na mtoto, kichomea taka na chumba cha kuhifadhia maiti.
Baada ya kuhakikishiwa na diwani kwamba enao la ujenzi liko tayari, Waziri Mkuu awetaka viongozi wa wilaya na tarafa hiyo wasimamie vizuri matumizi ya fedha hizo zitakapowasilishwa ili wananchi wapate huduma haraka.
Mapema, Mbunge Bindyaguze alisema wananchi wake wanahitaji kupatiwa vitambulisho vya taifa, na akaomba ahadi ya serikali ya kujenga KM. 5 za lami itekelezwe.