Meneja biashara wa kampuni ya PASS Leasing Tz Ltd,Maria Wambura akizungumza katika halfa hiyo ya kukabithi trekta kwa wakulima katika viwanja vya nanenane Themi Njiro.

Meneja biashara kutoka kampuni ya PASS Leasing Tz Ltd,Maria Wambura akikabithi ufunguo wa trekta kwa mmoja wa wakulima hao jijini Arusha
Julieth Laizer,Arusha .
Kampuni ya PASS Leasing Ltd inayomilikiwa na PASS TRUST imetoa mkopo wa trekta 4 kwa wakulima zenye thamani ya zaidi ya shs Milioni mia mbili kwa ajili ya kusaidia wakulima kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa kukabithi trekta hizo kwa wakulima hao katika maonyesho ya nanenane Themi Njiro, Meneja biashara wa kampuni ya PASS Leasing Tz Ltd,Maria Wambura amesema kuwa,lengo la kampuni hiyo kusaidia sekta ya kilimo kwa kutoa mashine na zana za kilimo ,uvuvi na ufugaji bila dhamana na kwa riba nafuu ili kuwawezesha wakulima kufikia malengo yao.
Amesema kuwa, lengo la kutoa mkopo wa zana hizo za kilimo kwa wakulima hao ni ili kuwawezesha kuweza kuendeleza shughuli zao za kilimo na kuondokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili hapo awali.
Wambura amesema kuwa, kwa kipindi cha miaka miwili tayari wamefikia wanufaika zaidi ya Mia sana wakiwemo wanawake na vijana ambapo wamekuwa wakishirikiana na wabia mbalimbali ambao ni wazalishaji wa zana za kilimo na makampuni.
“Trekta hizi tunazokabithi kwa wakulima hawa leo vimekatiwa bima na lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuunga mkono serikali katika maswala zima la kilimo katika kuhakikisha wakulima wanaondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili. “amesema Wambura.
Naye Meneja wa kanda ya kaskazini kutoka PASS -TRUST ,Hellen Wakuganda amesema kuwa,hicho ni chombo kilichoanzishwa mwaka 2000 ili kuchochea uwekezaji na kukuza kilimo cha biashara na sekta zinazohusika .
Amesema kuwa, dhamira ya asasi ya PASS inawajibika katika utoaji wa huduma za maendeleo ya kilimo cha biashara na fedha kwa wafanyabiashara wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kuwaunganisha katika taasisi za fedha .
Wakuganda amesema kuwa,wamekuwa wakiwasaidia wakulima kuandaa andiko la kibiashara na kupeleka kwenye mabenki na hatimaye kuweza kupewa mikopo huku wao wakiingia jukumu la kuwadhamini .
Kwa upande wa Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Arusha ambaye ni Afisa kilimo wa mkoa ,Daniel Loiruck akizungumza wakati wa kukabithi trekta hizo ameipongeza kampuni hiyo kwa namna ambavyo inaiunga serikali mkono katika juhudi za kilimo kwa kuwasaidia wakulima huku akiwataka kuendelea na juhudi hizo na kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Nao Wakulima waliokabithiwa trekta hizo waliishukuru kampuni hiyo kwa namna ambavyo imewasaidia kwani wameweza kujikwamua kiuchumi kwa kupata zana hizo za kisasa kwa ajili ya kilimo bora na chenye tija.