NAIBU Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha Dkt. Godwin Mollel amebainisha kuwa Serikali tayari imeingiza zaidi ya Bilioni 3.5 kwenye akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha ambayo itatumika kujenga shule ya wasichana ya kimkoa ya mchepuo wa Sayansi itayoanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ili watoto wa Mkoa wa Kilimanjaro wapate fursa ya kupata elimu bora ya Sayansi.
Dkt. Mollel amesema hayo, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ya ujenzi wa madarasa ya shule za Sekondari Sanya juu na Oshara zilizopo katika Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema, katika Wilaya nzima ni kata ya Mitimirefu ndio bado haina shule, huku akisisitiza kama mwakilishi wa wananchi ndani ya miezi mitatu atahakikisha kata hiyo inapata milioni 600 kwaajili ya ujenzi wa shule yake ili kuondoa changamoto kwa wanafunzi ya kutembea mpaka kata nyingine ili kupata elimu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa wanafunzi shule ya Sekondari Sanya juu amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Siha kwa kuendelea kuwaletea maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya yenye ubora na kuahidi kumsemea mazuri kwa wananchi wengine juu ya mambo makubwa aliyoyafanya kwa muda mfupi.
Sambamba na hilo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wanafunzi hasa kwenye suala la elimu bure na kuwajengea shule na madarasa mapya, huku akisisitiza kama wanafunzi wataendelea kumuunga mkono kwa kusoma kwa juhudi ili kufikia malengo.
Pia, amempongeza Mhe. Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha kwa ujenzi wa madarasa hayo huku akimkumbusha kuongeza walimu hasa walimu wa Sayansi kwani ujenzi huo wa madarasa utapelekea ongezeko la wanafunzi wa masomo ya Sayansi.