Serikali inaendelea kuboresha sera na sheria za haki za binadamu nchini ikiwemo sheria za habari pamoja na haki ya kisiasa na Demokrasia nchini kwa maslahi mapana ya taifa kwa ujmla.
Ameyasema hayo leo Desemba 8,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu Wizara ya Katiba na Sheria Ngasero Sarakikya katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Miikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere JNICC Jijini Dar es Salaam.
Amesema haki za binadamu ni chanzo cha amani hivyo serikali ina wajibu wa kuheshimu na kuthamini haki za binadamu.
“Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ili wananchi waendelee kunufaika na uhuru wa kutoa maoni na haki ya kutoa taarifa “. Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga ameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaovunja haki za binadamu lakini pia jamii kuwajibika kulinda haki za binadamu.
Aidha amesema Juhudi madhubuti zinahitajika kupunguza masuala ya mauaji ikiwa ni pamoja na kuboresha masuala ya upepelezi na mahakama lakini pia kuongeza uelewa kwa umma.
“Wao kama asasi za kiraia waongeze juhudi za kuongeza uelewa kwa umma juu ya utaratibu za kisheria na masuala ya haki za binadamu”. Amesema Wakili Henga
Ameongeza kwamba “Haki ya kuwa huru dhidi ya ukatili, ukatili wa watoto umekuwa mkubwa sana na mbaya zaidi ukatili huo unafanywa na watu wa karibu, akiwemo baba mdogo, babu, baba mzazi, mjomba n.k , hivyo tunatakiwa kuwalinda watoto”