******************
Zillipa Joseph, Katavi
Wakazi wa Katavi wameanza kuchukua hatua ya kupiga vita udumavu kwa watoto licha ya kuwa mkoa huo una uwezo mkubwa wa kuzalisha vyakula ambavyo vianishia kuuzwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria pamoja na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na Burundi.
Mkoa wa Katavi kwa sasa unatajwa kuwa na asilimia 33.3 ya watoto wenye lishe duni hali inayoelezwa kusababishwa na wakazi wa mkoa huo kutokuwa na uelewa wa kutosha wa namna ya kulisha watoto vyakula vya makundi mchanganyiko.
Pamoja na vyakula vinavyopatikana kwa wingi katika mkoa wa Katavi ni mahindi, mpunga, karanga, ufuta, choroko, maharagwe, dengu, mihogo, viazi vitamu na ulezi.
Aidha wakazi wa Katavi pia ni wafugaji wakubwa wa nyuki na hivyo kufanya upatikanaji wa asali kuwa wa kutosha pamoja na ufugaji wa ng’ombe na mbuzi.
Hatua za kupiga vita udumavu sasa zimefika katika makanisa ambapo jumapili hii mchungaji Ibrahim Swalo wa kanisa la Moravian mjini Mpanda alialikwa kutoa neno katika katika la Anglican Kristu Mfalme na kutoa somo kuhusu lishe.
Mchungaji Swalo amesema pengine hali ya lishe ilivyofikia mkoani katavi ni kutokana na siku hizi kutokuwa na somo la sayansi kimu lililokuwa limejikita katika kuelimisha jamii juu ya sayansi ya kiini cha maisha na uhai
Ameeleza kuwa mama mjamzito ni lazima ale vyakula vynye lishe bora kwa lengo la kuhakikisha mtoto aliye tumboni anajengeka vizuri kuanzia kiakili mpaka mpaka kimwili.
Aliwaeleza wakristo waliohudhuria kwenye ibada hiyo kuwa ubongo wa mtoto unakuwa hadi kufikia asilimia 90 pale anapofikisha miaka nane hivyo ni wajibu wa baba na mama kuhakikisha ubongo wa mtoto unatengenezwa vizuri kuanzia akiwa angali tumboni.
Amesema udumavu unasababisha mtoto anapokuwa mtu mzima kutokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na hivyo kupelekea kuwa na uzito mkubwa katika kufanya maamuzi mbalimbali ya maisha yake.
Aidha mch. Swalo Aliwasisitiza waumini kuhakikisha wanazingatia lishe bora kwa watoto ili kuepuka hali hiyo na hasa kwa wakati huu ambapo watu wanaanza kujiandaa na msimu wa kilimo kuacha tabia ya kutekelekeza watoto kuwaacha wajilee wenyewe angali wao wakienda vijijini kwenye kilimo kwa zaidi ya miezi mitatu hadi sita.
Baadhi ya waumini waliohudhuria ibada hiyo wamekiri kuwepo kwa tabia ya kuwaacha watoto wajilee wenyewe katika kila msimu wa kilimo.
Wamesema hali hiyo inasababishwa na wakazi wengi wa Katavi kutegemea Zaidi shughuli za kilimo.
Aidha kumekuwa na matamasha ya uandaaji vyakula vya lishe yanayosimamiwa na maafisa lishe yanayolenga kufundisha jamii namna bora ya kuandaa vyakula vya watoto