Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma Waziri Dkt, Pembe leo, tarehe 04.11.2026, amefanya mahojiano na kituo cha Televisheni cha Channel Ten, kuhusiana na Kiwanja cha Afcon Fumba na Mafunzo mbalimbali, ikiwemo AI, mafunzo ambayo yamefanyika Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.
…………
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma, amesema Wizara inaendelea kuwajengea uwezo Waandishi wa habari, kwa kutoa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kutumia teknolojia mpya katika ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa habari kwa usahihi kwa jamii.

Waziri Dkt, Pembe Amesema hayo wakati akifanya mahojiano na kituo cha televisheni cha Channel Ten yaliyofanyika ofisi za Wizara  Migombani,

Àmesema  kuwa Wizara imeandaa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari kwa kushirikiana na taasisi ya China Africa AI Media yanayolenga  kuwajengea ujuzi wa matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence – AI) katika kazi zao za kila siku.

Dkt,Pembe Amesema kupitia mafunzo hayo, waansishi wa habari watapata uelewa mpana wa matumizi sahihi ya teknolojia hiyo katika kurahisisha kazi zao na kuhakikisha ujumbe unaofikishwa kwa jamii unakuwa sahihi na kuleta  tija.

Aidha, amesema Waandishi wa habari watakaohitimu mafunzo hayo watakuwa na jukumu la kuwafundisha wenzao kutoka vyombo vingine vya habari ambavyo havijapata fursa ya kushiriki mafunzo hayo, ili kuongeza wigo wa uelewa na matumizi ya teknolojia hiyo katika tasnia ya habari.

Waziri Dkt ,Pembe Amesisitiza kuwa Wizara ina jukumu la kusimamia na kuhakikisha upatikanaji wa habari sahihi kwa jamii, huku ikiendelea kutoa elimu kwa wanahabari kuhusu umuhimu wa kuzingatia weledi, maadili na usahihi wa taarifa ili kuepuka habari za upotoshaji.

Akizungumzia Maandalizi ya Afcon amesema Mradi wa Afcon Fumba Umefikia asilimia 87 na Ujenzi wa Miundombinu ya nje inayozinguka Uwanja Umefikia asilimia 80 na unatarajiwa Ifikapo tarehe 31 Disemba 2026 kukabidhiwa kwa Serikali.        
 
Waziri Dkt, Pembe ameeleza kuwa Utekelezaji wa Ujenzi wa Mradi wa Afcon Fumba ni  maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi na Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya    2025-2030.