Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesema ujenzi wa kiwanda cha mbolea ya chumvichumvi kinachotumia gesi asilia katika Wilaya ya Mtwara Vijijini umeingia katika hatua za awali, baada ya kupatikana kwa mwekezaji wa kampuni ya Jundin Holding Limited.

Kiwanda hicho kinajengwa katika Kijiji cha Pembamvita, Kata ya Mayanga, Mtwara Vijijini, kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 150, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030.

Akijibu Swali Na. 110 la Mbunge wa Mtwara Vijijini, Arif Suleiman Premji, aliyetaka kujua lini kiwanda hicho kitajengwa kama ilivyoainishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga alisema Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imefanikiwa kupata mwekezaji aliyeonesha nia ya kutekeleza mradi huo.

“Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imepata mwekezaji wa kampuni ya Jundin Holding Limited aliyeonesha nia ya kujenga kiwanda cha mbolea ya chumvichumvi kitakachotumia gesi asilia,” alisema Waziri huyo.

Alisema kampuni hiyo tayari imepata eneo la kutekeleza mradi huo katika Kijiji cha Pembamvita, Kata ya Mayanga, Wilaya ya Mtwara Vijijini, lenye ukubwa wa ekari 150, na kwa sasa ipo katika hatua za awali za ujenzi wa kiwanda hicho.

Katika hatua nyingine, Serikali imesema inaendelea kuhamasisha wawekezaji wengine kujitokeza kwa ajili ya kujenga viwanda vitakavyoweza kuzalisha mbolea nchini.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uwekezaji katika sekta ya uzalishaji wa mbolea na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa shughuli za kilimo nchini.