Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamisi Mwinjuma, akizungumza na wageni wakati wa hafla ya uzinduzi wa Expect More katika Hoteli ya Serena, akiipongeza DStv kwa jitihada zinazopanua upatikanaji wa maudhui bora ya ndani na kutoa thamani zaidi kwa watazamaji wa Tanzania.

Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania,Sophie Tchatchoua, akihutubia wageni wakati wa hafla ya uzinduzi wa Expect More katika Hoteli ya Serena, akisisitiza thamani zaidi, maudhui mengi zaidi ya ndani, na burudani iliyoboreshwa kwa wateja wa DStv.

Mheshimiwa Hamisi Mwinjuma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mkurugenzi wa Bodi ya MultiChoice Tanzania, Nehemiah Mchechu, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu MultiChoice Tanzania, Sophie Tchatchoua, wakishuhudia uzinduzi rasmi wa Expect More; hatua mpya ya ujasiri inayowaletea Watanzania thamani zaidi, maudhui bora ya ndani, na burudani zaidi.
Mheshimiwa Hamisi Mwinjuma, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nehemiah Mchechu, Mkurugenzi wa Bodi ya MultiChoice Tanzania, pamoja na Sophie Tchatchoua, Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania, wakifurahia pamoja na waigizaji mahiri wa tamthilia mpya ya kizalendo KARATA wakati wa hafla ya uzinduzi wa Expect More; tukio lililoashiria hatua ya kujivunia katika kuendeleza simulizi za Kitanzania na kukuza ubora wa maudhui ya ndani.
…………….
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kuimarisha mapambano dhidi ya uharamia wa maudhui, ikieleza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha ukuaji wa sekta ya ubunifu, uwekezaji na uzalishaji wa maudhui bora nchini.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Pata Zaidi” ya DStv Tanzania, ambapo amewataka wadau wa sekta ya utangazaji kushirikiana katika kulinda haki miliki na kuhakikisha mazingira ya ubunifu yanakuwa endelevu.
Mwinjuma alisema uharamia wa maudhui unadhoofisha mnyororo wa thamani unaowezesha uundaji, usambazaji na ubunifu wa maudhui, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kushirikiana kukabiliana na biashara hiyo haramu.
“Uharamia wa maudhui unadhoofisha mnyororo wa thamani unaosaidia uundaji, usambazaji na ubunifu wa maudhui. Ni lazima tushirikiane kulinda haki miliki na kujenga mazingira yatakayowezesha ubunifu na uvumbuzi kustawi,” alisema.
Alisema ulinzi wa haki miliki ni muhimu katika kuhakikisha wabunifu, watangazaji na wawekezaji wanapata stahiki zao, hali itakayowahamasisha kuendelea kuzalisha maudhui yenye ubora na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya sekta ya ubunifu.
Aidha, Naibu Waziri aliipongeza MultiChoice Tanzania kwa mchango wake katika kukuza maudhui ya ndani na kuendeleza sekta ya ubunifu nchini, akibainisha umuhimu wa uwekezaji katika maudhui yanayowakilisha utamaduni na simulizi za Kitanzania.
Katika hafla hiyo, DStv Tanzania ilitangaza maboresho makubwa ya huduma zake kupitia kampeni ya “Pata Zaidi”, ikiwemo kupunguza idadi ya vifurushi kutoka sita hadi vinne pamoja na kupunguza bei kwa lengo la kuwapatia Watanzania burudani bora kwa gharama nafuu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania, Sophie Tchatchoua, alisema kampeni hiyo inalenga kuongeza thamani kwa wateja na kuwezesha watu wengi zaidi kupata burudani ya kiwango cha juu kupitia vifurushi vilivyoboreshwa.
“Pata Zaidi ni kuwapatia wateja wetu thamani zaidi kupitia vifurushi vilivyoboreshwa, bei nafuu zaidi, maudhui mengi ya ndani na huduma zinazozingatia mahitaji ya watazamaji wa Tanzania,” alisema Sophie.
Alisema maboresho hayo yanalenga kuimarisha uzoefu wa wateja na kuongeza upatikanaji wa maudhui mbalimbali yanayokidhi mahitaji ya watazamaji wa Tanzania, ikiwemo michezo, filamu, tamthilia na vipindi vya watoto.
Miongoni mwa maboresho yaliyotangazwa ni kuanzishwa kwa chaneli ya SuperSport Kiswahili, inayotoa matangazo ya michezo na uchambuzi kwa lugha ya Kiswahili, hatua inayolenga kuwafikia zaidi mashabiki wa michezo wanaopendelea lugha hiyo.
Pia, DStv imeongeza maudhui ya watoto kupitia Ubongo Kids, huku ikiimarisha uwekezaji katika maudhui ya ndani kwa kutambulisha tamthilia mpya ya KARATA, inayolenga kuendeleza simulizi za Kitanzania na Kiafrika.
Katika maboresho ya vifurushi, DStv imetangaza kifurushi kipya cha DStv Sports kitakachowapatia wapenzi wa michezo maudhui mbalimbali kwa Sh 50,000, kutoka bei ya awali ya Sh 118,000.
Kwa upande wa mashabiki wa Ligi Kuu ya England (EPL), kifurushi kipya cha DStv Select kitawawezesha kutazama mechi za ligi hiyo kwa Sh 25,000, badala ya Sh 68,000 zilizokuwa zikilipwa kupitia kifurushi cha zamani cha Compact.
Aidha, wapenzi wa maudhui ya nyumbani yakiwemo tamthilia, vichekesho na filamu wataweza kuyapata kupitia kifurushi kipya cha DStv Starter kwa Sh 15,000, kutoka bei ya awali ya Sh 27,500.
MultiChoice Tanzania imesema itaendelea kuongeza maudhui mengi zaidi ya Kiswahili na yanayozalishwa nchini katika majukwaa yake, ikiwemo tamthilia ya KARATA inayotarajiwa kuanza kurushwa Novemba 2026.
Maboresho hayo yanaelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa DStv wa kuongeza thamani kwa wateja, kupanua upatikanaji wa burudani na kuimarisha nafasi ya maudhui ya ndani katika sekta ya utangazaji nchini.

