Na.Sophia Kingimali, Dar es Salaam

BUNGE katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu Afrika limetakiwa kuimarisha usimamizi na uwajibikaji wa Serikali ili kuhakikisha ahadi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, amani na usalama zinatafsiriwa katika vitendo badala ya kubaki kwenye sera na mipango.

Wito huo umetolewa leo Novemba 3,2026 na Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula, wakati wa mdahalo kuhusu nafasi ya wanawake katika kulinda amani kwenye Mkutano wa Wanawake Wabunge wa Ukanda wa Maziwa Makuu Afrika unaoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema nchi nyingi za Afrika zimeweka sera, sheria na mifumo ya kikanda inayolenga kuendeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama, lakini utekelezaji, upatikanaji wa fedha na uwajibikaji bado ni changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.

Aidha amezitaka Bunge kuzitaka Serikali kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Mipango ya Kitaifa ya Wanawake, Amani na Usalama, zikionesha fedha zilizotengwa, hatua zilizofikiwa na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wake.

Aidha, ameeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la ukatili dhidi ya wanawake unaochochewa na teknolojia, hususan mashambulizi kupitia mitandao ya kijamii dhidi ya wanawake wanaowania nafasi za uongozi wa kisiasa, akisema hali hiyo inakatisha tamaa ushiriki wao katika shughuli za umma.

Amewataka wabunge na wizara husika kuimarisha mifumo ya ulinzi ili wanawake waweze kushiriki katika michakato ya kisiasa bila kukabiliwa na vitisho, ubaguzi wala unyanyasaji.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Judith Tuluka, amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuongeza wanawake kwenye nafasi za uongozi, bado changamoto za ubaguzi wa kijinsia na ukatili zinaendelea kuwazuia kushiriki kikamilifu katika ngazi za maamuzi.

Amesema kwa sasa wanawake wanachukua asilimia 33.6 ya nafasi ndani ya Baraza la Mawaziri la nchi hiyo, huku wanawake 17 wakishikilia nyadhifa za uwaziri, zikiwamo wizara muhimu za Mambo ya Nje, Elimu ya Taifa na Ustawi wa Jamii.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya maamuzi ya kisiasa ya kuongeza uwakilishi wa wanawake katika uongozi, akibainisha kuwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966, DRC imepata mwanamke kushika nafasi ya Waziri Mkuu.

Amesisitiza kuwa wanawake hawapaswi kunyimwa nafasi za uongozi kwa sababu ya jinsia yao, bali uwezo, ujuzi na sifa za mtu vinapaswa kuwa vigezo vya kupewa dhamana ya uongozi.

Akizungumzia uzoefu wake tangu alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, amesema mwanzoni baadhi ya watu walitilia shaka uwezo wake wa kuiongoza nchi iliyokuwa katika mazingira ya vita na changamoto mbalimbali.

Ameongeza kuwa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi kunahitaji uwekezaji katika elimu, mafunzo ya ufundi na uongozi, huku wanaume wakihamasishwa kushiriki kupinga ubaguzi kupitia dhana ya uanaume chanya (Positive Masculinity).

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dk. Zeyana Hamid, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), amesema Tanzania bado inakabiliwa na pengo la uwakilishi wa wanawake katika ngazi za serikali za mitaa licha ya kuwa na uwakilishi wa Bunge unaokaribia asilimia 40.

Amesema wanawake madiwani ni takribani asilimia tisa, hali inayoonesha umuhimu wa kupanua juhudi za usawa wa kijinsia hadi kwenye halmashauri na kata ambako maamuzi mengi yanayogusa maisha ya wananchi hufanyika.

Ameongeza kuwa mafanikio ya usawa wa kijinsia hayapaswi kupimwa kwa idadi ya wanawake walio katika nafasi za uongozi pekee, bali pia mchango wao katika maamuzi, utekelezaji wa sera na ugawaji wa rasilimali, akibainisha kuwa kwa sasa kamati saba za Bunge zinaongozwa na wanawake.