Paris, 1 Novemba 2026,
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, kwa kushirikiana na Exodus Brokerage Services, umeratibu mafunzo ya uwekezaji kwa Watanzania wanaoishi nchini humo, yakilenga kuongeza uelewa wa fursa zilizopo katika masoko ya fedha na mitaji nchini Tanzania.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Yakubu, na kuwashirikisha Watanzania waliohudhuria katika Makazi ya Balozi jijini Paris pamoja na wengine waliojiunga kwa njia ya mtandao.
Wasilisho kuu lilitolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Exodus Brokerage Services, likijikita katika uwekezaji nchini Tanzania kwa Watanzania wanaoishi Ufaransa na namna masoko ya mitaji yanavyoweza kuwaunganisha na fursa za kiuchumi nyumbani.
Kwa kuwakutanisha wanadiaspora na wataalamu wa uwekezaji, mafunzo hayo yalitoa jukwaa la kujifunza na kujadiliana kuhusu namna ya kufanya maamuzi ya uwekezaji kwa kuzingatia taarifa na uelewa sahihi.
Ushirikiano huo unaonesha nafasi ya Ubalozi katika kuwaunganisha Watanzania waishio nje ya nchi na utaalamu pamoja na fursa za uwekezaji nchini Tanzania, ili kuimarisha ustawi wao na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.


