Diwani wa Kata ya Sokon One,Muksin Juma wakati akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha

Mkurugenzi wa kituo cha Karimu Daycare ,Ayoub Mswahili akizungumza na wazazi pamoja na wanafunzi hao

………..

Na Happy Lazaro, Arusha

WAZAZI nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwekeza kwenye elimu ya watoto wakiwa tangu wadogo kwa kuwapeleka kwenye vituo vinavyotoa elimu ya awali ili kuwejengea msingi mzuri ya kupenda elimu wakiwa tangu wadogo.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Diwani wa Kata ya Sokon One,Muksin Juma wakati akizungumza kwenye mahafali ya nne ya wanafunzi wa elimu ya awali katika kituo cha Karimu Day Care ambapo jumla ya wanafunzi 27 wamehitimu elimu ya awali.

Muksin amewapongeza waanzilishi wa Kituo cha Karimu kwa kuwekeza katika elimu ya watoto wadogo na kujiandaa kupanua huduma zao kwa kuwa na malengo ya kuanzisha shule ya msingi, akitabiri kuwa shule hiyo itakuwa na mvuto mkubwa kwa wazazi kutokana na msingi unaojengwa kupitia elimu ya awali.

Amesema juhudi zinazofanywa na uongozi wa kituo hicho zinaonesha dhamira ya kuchangia maendeleo ya jamii kupitia elimu, akiwataka kuendeleza mipango yao kwa kuzingatia mahitaji ya watoto na ukuaji wa idadi ya wanafunzi watakaohitaji huduma hiyo.

Aidha ameahidi kufuatilia changamoto ya ukosefu wa chumba cha kompyuta na vifaa vyake katika kituo hicho, na kusema atachunguza mahitaji yaliyopo na kuangalia namna anavyoweza kutoa mchango kulingana na uwezo wake.

Aidha, amewataka wananchi wa kata hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya mvua, hususan wanaoishi mabondeni na karibu na mikondo ya maji, kwa kuhakikisha mifereji inasafishwa ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kupunguza hatari ya mafuriko.

Amesema wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanapaswa kuzingatia maelekezo ya serikali kupitia viongozi wa mitaa na mabalozi, ikiwemo kuhamia kwa muda katika maeneo salama endapo hali itahitaji kufanya hivyo.

Naye Mkurugenzi wa kituo hicho cha Karimu Day Care,Rehema Kindoi amesema kuwa kituo hicho kimekuwa kikitoa huduma ya malezi ya watoto wadogo kuanzia siku moja hadi miaka mitano ambapo wamekuwa wakiwapa malezi bora kwa kufuata mwongozo wa malezi ya watoto.

Amesema kuwa,wamekuwa wakifundisha kwa mtaala wa kiingereza na watoto wakitoka hapo wana uwezo wa kujiunga na shule yoyote kutokana na elimu nzuri waliyopatiwa kituoni hapo.

Rehema ametumia nafasi hiyo kuwataka wazazi kuwekeza zaidi kwenye elimu ya watoto wao kuanzia elimu ya awali na makuzi ili wanapofika darasa la kwanza waweze kufanya vizuri kwani kuna tofauti kubwa kati ya mtoto anayepitia elimu ya awali na yule anayeenda darasa la kwanza moja kwa moja.

“Nawaomba sana mkitumie kituo hiki.cha Karimu daycare kwani kimekuwa kikiwaandaa watoto vizuri sambamba na kufundisha somo la maadili ambalo limemomonyoka kwa kiasi kikubwa kwenye jamii inayotuzunguka .”amesema Rehema .

Naye Mratibu wa Elimu wa Kata ya Sokon One amesema waanzilishi wa Kituo cha Karimu wameamua kuwekeza katika elimu ya watoto wadogo kwa lengo la kuijengea jamii imani na kuweka msingi wa maisha bora ya baadaye kwa watoto.

Amesema hatua ya mwanzilishi wa kituo hicho, ambaye ana shahada ya uzamivu (PhD), kuamua kuanzisha huduma ya elimu ya awali ni jambo linalostahili pongezi kwa kuwa linaonesha dhamira ya kutumia maarifa yake katika kuisaidia jamii.

Mratibu huyo ameeleza kufurahishwa na uwezo unaooneshwa na watoto katika kituo hicho, akisema baadhi yao wanaonesha uelewa na uchangamfu unaoashiria umuhimu wa kuwapatia mazingira bora ya kujifunzia tangu wakiwa wadogo.