Na.Sophia Kingimali.
Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini (RUJAT) kimeweka kipaumbele katika kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari kuibua na kuandika habari zinazogusa maisha ya wananchi wa vijijini, ili changamoto na fursa zinazowakabili zipate nafasi katika vyombo vya habari.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Charles Meena, aliyechaguliwa tena kuongoza chama hicho kwa kipindi kingine cha miaka minne katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 31, 2026, jijini Dodoma.
Meena, ambaye ni Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya Media Brains na mmoja wa waasisi wa RUJAT, amesema katika kipindi chake kipya atahakikisha habari za vijijini zinapewa uzito unaostahili katika vyombo vya habari ili kuhakikisha sauti ya watu wa vijijini inasikika.
Amesema lengo ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi wa vijijini pamoja na fursa zilizopo katika maeneo hayo zinafahamika na jamii na kufikishwa kwa mamlaka zinazohusika kwa ajili ya hatua stahiki.
Amesisitiza kuwa ili kufikia lengo hilo, chama kinahitaji kuimarisha uwezo wa wanachama wake, hususan katika ujuzi wa kuandaa na kuandika habari zenye ubora zinazozingatia maslahi ya umma.
Amesema pia atashirikiana na viongozi wenzake kukijengea uwezo RUJAT na kusimamia utekelezaji wa malengo yake ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Meena alitangazwa mshindi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Felix Mwakyembe, baada ya kupata kura 74 kati ya 77 zilizopigwa, akiwashinda wagombea wenzake Rashid Abdullah Mtagaluka na Andrea Ashery Ngolola.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Meena amesema kura alizopata ni dhamana kubwa kwake na ameahidi kuitumia nafasi hiyo kuwatumikia wanachama kwa moyo wote.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Hamida Ramadhan kutoka Dodoma amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.
Kwa upande wa nafasi ya Katibu, Prosper Laurent Kwigize kutoka Kasulu mkoani Kigoma amechaguliwa tena baada ya kupata kura 76 kati ya 77 zilizopigwa.
Aidha, Zena Mohamed Chitwanga amechaguliwa kuwa Mweka Hazina wa RUJAT, huku wajumbe saba waliochaguliwa kuunda Kamati Tendaji wakiwa Musa Juma Siwayombe, Devotha Martine Paul, Malunde Kadama, Rashid Abdullah Mtagaluka, Anna Robi, Andrea Ashery Ngolola na Fadhili Abdallah Mwangamola.
Kwa mujibu wa mabadiliko ya Katiba yaliyopitishwa na wanachama wa RUJAT, uongozi mpya utaongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka minne kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine.

