Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Akifungua Jukwaa la Miundombinu Afrika na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 uliofanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Agosti 05,2026.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa viongozi wa Afrika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kuchochea biashara, kuvutia uwekezaji na kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Akifungua Jukwaa la Miundombinu Afrika na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 uliofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema maendeleo ya bara hayawezi kupimwa kwa sera au mipango pekee, bali kwa matokeo yanayoonekana kupitia uboreshaji wa barabara, reli za kisasa, madaraja, bandari, nishati na teknolojia.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa viwanda, jumuishi na unaotegemea ubunifu pamoja na ujuzi, huku ikiimarisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya miundombinu.
Rais Samia amesema nafasi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inaifanya nchi kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi za ukanda huo, hususan Burundi, Rwanda, Uganda, Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam pamoja na miundombinu mingine ya usafiri na usafirishaji ili kuongeza ushindani wa uchumi na kurahisisha biashara ndani na nje ya nchi.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Afrika inapaswa kuongeza thamani ya rasilimali zake badala ya kuendelea kuuza malighafi, hatua ambayo itasaidia kuongeza ajira, kukuza viwanda na kuimarisha uchumi wa bara.
Akizungumzia sekta ya nishati, amesema matumizi ya gesi asilia yana mchango mkubwa katika kuongeza usalama wa nishati, kusaidia ukuaji wa viwanda na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Rais wa Kenya, Prof. Kithure Kindiki, amesema mafanikio ya miradi mikubwa ya maendeleo yanategemea uwepo wa uongozi madhubuti wa kisiasa, sera thabiti na mipango ya muda mrefu, huku akizitaka nchi za Afrika kujenga uwezo wa kitaalamu, kutumia mifumo bunifu ya fedha na kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Africa50 ambaye pia ni Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na nchi za Afrika kubadilisha fursa za miundombinu kuwa miradi inayoweza kufadhiliwa na kutekelezwa kwa ufanisi.
Katika mkutano huo pia kulifanyika mjadala uliowashirikisha mawaziri kutoka Tanzania, Msumbiji, Nigeria na Senegal kuhusu maendeleo ya sekta za nishati na viwanda. Ilielezwa kuwa zaidi ya Waafrika milioni 600 bado hawana huduma ya umeme, huku Tanzania ikiongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kutoka asilimia sita mwaka 2021 hadi asilimia 28 mwaka 2026.
Katika hatua nyingine, Tanzania ilisaini makubaliano ya kupanua huduma za matibabu ya figo, kuendeleza miundombinu ya usafirishaji wa umeme kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na kuongeza matumizi ya gesi asilia viwandani.
Makubaliano hayo yanahusisha Africa50, Wizara ya Afya, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na kampuni ya TAQA Arabia.
Rais Samia ameipongeza Africa50 kwa kuendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya miundombinu barani Afrika na kusisitiza kuwa utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa ndio utakaowezesha wananchi kupata manufaa ya uwekezaji huo.

