Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Kazi,Ajira na Mahusiano) Deus Sangu ( katikati) akikata utepe kufungua mradi wa mabweni mapya mawili kwa ajili ya wavulana wanaosoma shule ya sekondari Mtanga iliyopo Kilwa Masoko hafla iliyofanyika 03 Agosti 2026 wakati akiwa katika ziara ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita mkoani Lindi.

*Ampongeza Rais Samia kwa Uwekezaji Sekta ya Elimu
Na. OWM (KAM), Kilwa Masoko
Viongozi wa halmashauri nchini wamekumbushwa kuanza maandalizi ya kuweka miundombinu wezeshi kukudhi mahitaji kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwqnza mwaka 2028 ambapo madarasa ya saba na la sita watahitimu kwa pamoja.
Aidha, amesisitiza kuwa maandalizi hayo yahusishe ujenzi wa madarasa, mabweni na miundombinu mingine muhimu ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata nafasi ya kuendelea na masomo bila changamoto.
Wito huo umetolewa wilayani Kilwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu tarehe 3 Agosti 2026 alipokuwa akizindua mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Mtangani, ambapo mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 362 na kueleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kwa kuwa ndiyo msingi wa ukombozi wa wananchi na maendeleo ya haraka ya Taifa.
Amefafanua kuwa, katika Wilaya hiyo, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.477 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu ya sekondari, hatua ambayo imeleta mageuzi makubwa katika miundombinu ya elimu na kuongeza fursa za wanafunzi kusoma katika mazingira salama na rafiki.
Kadhalika, Mhe. Sangu pia ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Lindi katika kusukuma mbele agenda ya maendeleo na kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo chanya kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kusini Hasnain Dewji amesema kuwa kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa, hivyo amewahakikishia wananchi wa Kilwa kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta hiyo muhimu.
Naye, Mkuu wa Shule ya Mtanga Hussein Kiwela, mradi huo wa ujenzi wa mabweni na miundombinu nyingine ya elimu itaongeza fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kupata elimu ya sekondari ya juu na kuwaandaa kujiunga na elimu ya juu pamoja na vyuo vya ufundi na mafunzo ya stadi mbalimbali.
“Kupitia uwekezaji huu, Taifa litaendelea kupata rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kuchangia kikamilifu katika maendeleo,” amesema
