NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Benjamin Sitta, ameongoza zoezi la kugawa unga wa lishe katika shule mbalimbali za Manispaa ya Iringa, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kupambana na udumavu na kuboresha afya ya watoto nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sitta alisema kuwa Rais Samia amesisitiza kuimarishwa kwa mpango wa lishe shuleni kupitia mkataba wa lishe ulioasisiwa mwaka 2022, ambao unahusisha wakuu wa mikoa na wilaya katika kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubisho vya kutosha.
“Lengo la Mhe. Rais ni kuwa na taifa la watu wenye afya bora. Ndiyo maana mikataba hii imesainiwa na utekelezaji unaendelea kwa kushirikiana na halmashauri. Huu unga wa lishe tuliogawa leo ni sehemu ya kuhakikisha kila mtoto, bila kujali mchango wa mzazi, anapata uji wenye virutubisho muhimu, ikiwemo Vitamin A kwa ajili ya uoni na afya ya macho,” alisema Mhe. Sitta.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Bi. Zaina Mlawa, alisema manispaa imetenga fedha kutoka posho za vikao na mapato ya ndani ili kuunga mkono juhudi za serikali na wazazi katika kuboresha lishe shuleni.
“Tumeamua kuwa mfano kwa kutenga bajeti ya manispaa kununua chakula cha lishe kwa shule zetu. Leo tunaanza na shule tano za msingi na sekondari, na hili zoezi ni endelevu,” alisema.
Naye Afisa Lishe wa Manispaa, Bi. Anzaeli Msigwa, alieleza kuwa unga huo una faida nyingi ikiwemo kuongeza hamu ya kula, kuimarisha kinga ya mwili, na kuimarisha uoni kutokana na wingi wa Vitamin A.
“Watoto hawa wanapokula vizuri, wanakaa darasani kwa utulivu na ufaulu unaongezeka mwaka hadi mwaka. Hivi sasa asilimia 70 ya wanafunzi wa manispaa wanapata chakula shuleni, na tunapambana kuhakikisha asilimia 30 iliyobaki inafikiwa,” alisema.
Msigwa aliongeza kuwa shule nyingi sasa zina bustani za mboga zinazosaidia kuongeza vitamini E na virutubisho vingine muhimu kwa afya ya watoto, hatua inayochochea mapambano dhidi ya utapiamlo na utoro.
Zoezi la ugawaji unga wa lishe limepokelewa kwa furaha na walimu pamoja na wanafunzi, huku wazazi wakihimizwa kuendelea kuchangia ili kuhakikisha kila mtoto anapata mlo kamili shuleni.




