Na Sabiha Khamis Maelezo 10.01.2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe. William Vangimembe Lukuvi, amesema Serikali ya awamu ya nane imeweka hitoria mpya ya kuanzisha Chuo cha Kimataifa ili kukuza sekta ya elimu nchini.
Ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa dakhalia za wanafunzi katika chuo cha Indian Institute of Technology Madrasa (IITM), ikiwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema uwepo wa tawi la chuo cha IITM ni sehemu ya kutekeleza dhamira ya viongozi wakuu wa nchi ya kuhakikisha kila kijana anapata elimu bora inayotambuliwa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuendeleza misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
“Uwekezaji huu katika elimu ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali katika kuyaenzi, kuyatunza na kuyaendeleza Mapinduzi, hasa katika kuhakikisha haki ya msingi ya kupata elimu bora kwa kila mtoto wa Kizanzibar,” amesema Mhe. Lukuvi.
Ameeleza kuwa Mapinduzi yameleta mabadiliko makubwa ya kijamii ikiwemo usawa wa upatikanaji wa elimu, tofauti na kipindi cha kabla ya Mapinduzi ambapo elimu ya juu ilikuwa fursa ya wachache kutokana na kukosekana kwa vyuo vikuu.
Mhe. Lukuvi amesema kuanzishwa kwa chuo cha IITM ni sehemu ya mageuzi ya elimu ya juu nchini, kikilenga kuzalisha wataalamu watakaokidhi mahitaji ya sasa na baadae, hususan katika nyanja za Akili Bandia (AI), Teknolojia ya Habari na Uchambuzi wa Takwimu (Data), sambamba na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa.
Aidha amewataka vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa ya uwepo wa Chuo cha International Institute of Technology and Management (IITM) ili kujiendeleza kielimu na kiujuzi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Taaluma, Dk. Mwanakhamis Adam Ameir, amesema mradi wa ujenzi wa dakhalia hizo ulianza kutekelezwa Mei 2024 na unatarajiwa kukamilika Machi 2026, kwa gharama ya shilingi bilioni 13.98.
Ameeleza kuwa mradi huo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji, ukihusisha ujenzi wa majengo manne ya dakhalia yenye jumla ya vyumba 24, kila chumba kikiwa na choo chake.
“Vyumba hivyo vimejengwa kwa viwango tofauti, vipo vya mtu mmoja mmoja na vingine vyenye uwezo wa kuchukua watu wawili kwa wakati mmoja,” amefahamisha Dk. Mwanakhamis.
Dkt. Mwanahamis ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa wanafunzi 96 kuishi katika dakhalia hizo na kupunguza changamoto ya uhaba wa nafasi za malazi kwa wanafunzi wa chuo hicho.
“Yatakapokamilika majengo haya, chuo kitakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi wengi zaidi ambao awali tulikuwa tunawaacha kutokana na uhaba wa malazi,” alisema.
Dk. Mwanakhamis amesema mradi huo pia utasaidia Serikali kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, kupitia uzalishaji wa wataalamu wengi katika sekta zinazohusiana na teknolojia za kisasa na uchumi wa kidijitali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’, Amour Yussuf Mmanga, amesema sekta ya elimu ilipewa kipaumbele mara tu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, ambapo Baraza la Kwanza la Mapinduzi lilitoa waraka wa kupanua wigo wa elimu kwa wananchi wote.
Amesema Rais wa Awamu ya Nane wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameendeleza juhudi hizo kwa kuongeza bajeti ya elimu na kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa miundombinu ya elimu, hali iliyopelekea kuimarika kwa sekta hiyo mijini na vijijini.




