Na Sophia Kingimali
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza rasmi matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili uliofanyika Oktoba/Novemba 2025, ambapo Takwimu zinaonesha kuwa wasichana wamefaulu zaidi kuliko wavulana, ambapo asilimia 90.10 ya wasichana wamefaulu ikilinganishwa na asilimia 87.59 ya wavulana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo,Januari 10,2026 Katibu Mtendaji Profesa Said Mohamed amesema upimaji huo ulihusisha wanafunzi waliokuwa wanatumia mifumo miwili ya mitaala, ikiwemo mtaala ulioboreshwa na mtaala wa awali. Kwa Darasa la Nne, wanafunzi wote walifanya upimaji kwa mtaala ulioboreshwa, huku kwa Kidato cha Pili baadhi ya wanafunzi wakifanya kwa mtaala wa awali na wengine kwa mtaala ulioboreshwa (Mkondo wa Amali), ambao uliendeshwa kwa mara ya kwanza katika ngazi hiyo.
Kwa upande wa Darasa la Nne, jumla ya wanafunzi 1,583,686 walijiandikisha kufanya upimaji, kati yao wanafunzi 1,490,377 walifanya upimaji huo sawa na asilimia 94.11. Matokeo yanaonesha kuwa wanafunzi 1,324,970 sawa na asilimia 88.91 wamefaulu na kuchaguliwa kuendelea na Darasa la Tano mwaka 2026, hali inayoonesha ongezeko la ufaulu wa asilimia 2.67 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Takwimu zinaonesha kuwa wasichana wamefaulu zaidi kuliko wavulana, ambapo asilimia 90.10 ya wasichana wamefaulu ikilinganishwa na asilimia 87.59 ya wavulana. Aidha, ubora wa ufaulu umeimarika, wanafunzi waliopata madaraja ya A hadi C wakiwa 62.48, ongezeko ikilinganishwa na asilimia 60.85 ya mwaka 2024.
Katika Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, jumla ya wanafunzi 898,718 walijiandikisha kufanya upimaji huo wakiwemo wa shule na wa kujitegemea. Kati yao, wanafunzi 811,575 wa shule walifanya upimaji sawa na asilimia 91.26, huku wanafunzi wa kujitegemea 7,437 sawa na asilimia 78.67 wakishiriki kikamilifu.
Profesa Said Mohamed amesema Baraza limefuta matokeo ya baadhi ya wanafunzi waliobainika kufanya udanganyifu au kuandika matusi kwenye skripti zao. Jumla ya wanafunzi 49 wa Darasa la Nne na 40 wa Kidato cha Pili walifutiwa matokeo kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Mitihani na Kanuni za Mitihani za mwaka 2016.
Akihitimisha taarifa hiyo, Profesa Said Mohamed ametoa pongezi kwa kamati za uendeshaji mitihani za mikoa na halmashauri, wakuu wa shule, wasimamizi na wasahihishaji kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya. Pia aliwapongeza wanafunzi wote kwa kuzingatia nidhamu na taratibu za mitihani katika kipindi chote cha upimaji huo.



