Na Ashrack Miraji Fullshangwe Blog
Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola, ametembelea vyanzo vitatu vya maji vilivyopo katika kata tatu tofauti jimboni humo kwa lengo la kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji na changamoto zinazowakabili wananchi, hususan kipindi hiki cha kiangazi.
Katika ziara hiyo, Mbunge Koola alitembelea chanzo cha maji cha Kizumbe kilichopo Kijiji cha Mshiri, Kata ya Marangu Mashariki; chanzo cha Kiwindo kilichopo Kijiji cha Komakundi, Kata ya Mamba Kaskazini; pamoja na chemchem ya Nsirwe iliyopo Kijiji cha Kimangara, Kata ya Mamba Kusini, ambavyo vyote ni chemchem za asili.
Ilielezwa kuwa chanzo cha Kiwindo kimekauka kabisa kutokana na athari za kiangazi, hali iliyosababisha wananchi wa maeneo hayo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, jambo lililomlazimu Mbunge huyo kuitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MUWASA) kuchukua hatua za dharura.
Ziara hiyo ilihusisha viongozi mbalimbali wakiwemo Diwani wa Kata ya Mamba Kusini, Mheshimiwa Reward Minja, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, wazee mashuhuri pamoja na viongozi na watumishi wa MUWASA ambao walitoa maelezo kuhusu hali ya vyanzo hivyo na changamoto za kiutendaji.
Kupitia ziara hiyo, changamoto kadhaa zilibainika na baadhi zilianza kufanyiwa kazi mara moja, huku pia ikibainika kuwepo kwa uzembe kwa baadhi ya watumishi wa ngazi ya chini wa MUWASA, hususan mafundi, kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mheshimiwa Koola aliuagiza uongozi wa MUWASA kuchukua hatua za haraka za muda mfupi kutatua changamoto zilizopo, huku akiahidi kuwasilisha bungeni hoja za kisera na kisheria ili Serikali iweze kutoa suluhisho la kudumu kwa tatizo la maji kwa wananchi wa Jimbo la Vunjo.




