NA DENIS MLOWE IRINGA
MBUNGE wa Iringa Mjini ameonyesha kusikitishwa na hali ya vivuko katika Manispaa ya Iringa, akisema kuwa idadi kubwa ya vivuko takribani vitano hadi sita havipitiki kabisa na kuwaumiza wananchi wanaovitegemea kwa safari za kila siku.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kata mbalimbali kuangalia miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi akiwa mtaa wa Ngeleli katika kata hiyo
mbunge Ngajilo alisema changamoto imekuwa ni wimbo wa muda mrefu, licha ya juhudi ndogo ndogo zilizowahi kuanza katika baadhi ya maeneo.
Amefafanua kuwa maeneo kama Makolongoni hayana hata miti ya kuvukia, hali inayowalazimu wananchi kuzunguka umbali mrefu kufika shuleni, kwenye makazi au katika shughuli zao za uzalishaji.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa matatizo kama haya ni madogo na yanapaswa kutatuliwa haraka ili nguvu ziwekezwe kwenye changamoto kubwa zinazowakabili wananchi.
Alikumbusha kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kutatua changamoto zinazowezekana ndani ya siku 100, akisema kuwa kama wasaidizi wake wanapaswa kuonyesha mfano.
Katika hatua ya kutatua tatizo hilo, ametoa agizo kwa ofisi yake ya mbunge, wasaidizi wake pamoja na mtendaji wa kata kuhakikisha kivuko hicho kinaanza kupitika ndani ya siku 14 kuanzia alipotangaza maelekezo hayo leo.
Ameagiza ushirikiano wa karibu kati ya ofisi ya mbunge na viongozi wa eneo husika ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na wananchi waanze kuvuka bila kero.
“Lazima tuwasaidie wananchi. Hili suala liishe sasa,” amesema mbunge huyo, akiahidi kuwa kufikia muda huo, changamoto hiyo itakuwa imetatuliwa.
Mbunge wa Iringa Mjini atembelea Kata ya Ruaha, aahidi suluhisho la haraka kwa changamoto za wananchi
Kwa upande wake akiwa katika ziara hiyo, Diwani Mbungu alieleza kuwa kivuko hicho ni muhimu kwa wananchi wa eneo hilo, wakiwemo wanafunzi wa Shule ya Msingi Ipogolo ambao hulazimika kukitumia kila siku.
Alisena kuwa Kwa muda mrefu kivuko hicho kimekuwa hatarishi na kimekuwa chanzo cha kuchelewesha wanafunzi kufika shuleni, hasa msimu huu wa mvua ambapo maji huzidi na kufanya eneo hilo kuwa hatari zaidi.
“Watoto hawana njia mbadala. Wasipovuka hapa wanalazimika kuzunguka umbali mrefu sana, jambo linalowachelewesha masomo,” alisema diwani Mbungu.
Aidha, Mbungu aliongeza kuwa wakazi wa eneo hilo pia wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji machafu yanayodaiwa kutoka kwenye baadhi ya viwanda ambayo hupitia katika mtaro unaokatiza pembezoni mwa makazi ya watu.
Alisema kuwa Maji hayo, kwa mujibu wa wakazi, yamekuwa chanzo cha magonjwa ya tumbo, muasho wa macho, pamoja na harufu kali inayozidi kuhatarisha afya zao.
Wakitoa ushuhuda, wananchi walieleza kuwa tatizo hilo limekuwa likiathiri maisha yao kwa muda mrefu, huku baadhi wakipata madhara makubwa kiafya.
Aidha, iliripotiwa kuwa hivi karibuni mama mmoja mkazi wa eneo hilo alipata ajali ya kuanguka na kuvunjika mguu kutokana na hali mbovu ya kivuko hicho, na bado anaendelea na matibabu.
“Huyo ni mtu mzima, sasa fikiria watoto. Ni hatari zaidi,” alisema diwani Mbungu akisisitiza umuhimu wa suluhisho la haraka.
Akijibu suala la maji machafu Mbunge wa Iringa Mjini aliishukuru serikali ya mtaa kwa kutoa taarifa za kina na kuahidi kuwa ofisi yake itashirikiana na mamlaka husika, ikiwemo halmashauri ya manispaa, kuhakikisha kwamba kivuko kinajengwa upya na chanzo cha maji machafu kinadhibitiwa kwa haraka iwezekanavyo
Mbunge pia amekagua miradi mingine ya maendeleo ikiwemo daraja la Cagrielo–Ipogolo, barabara ya Kasessela Road na miradi ya elimu katika Shule za Msingi J.J. Mungai na Ipogolo, ambazo zimepokea fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati.




