
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. David Homeli Mwakyusa akiwatunuku wahitimu wa digrii za ubobezi na digrii ya uzamivu katika Mahafali ya 19 ya MUHAS yaliyofanyika leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Makamu Mkuu wa MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa akitoa taarifa ya utendaji wa chuo katika Mahafali ya 19 ya MUHAS yaliyofanyika leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Baraza la MUHAS , Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika Mahafali ya 19 ya MUHAS.

Makamu Mkuu wa taaluma MUHAS Prof. Emmanuel Balandya akizungumza katika Mahafali ya 19 ya Chuo hicho.
Mwakilishi wa wahitimu wa Shahada za awali MUHAS Jackline G. Malavanu akitoa hotuba
Mwakilishi wa wahitimu wa Shahada za Uzamili MUHAS Alfred Chibwe akitoa hotuba


Baadhi ya wahitimu wa Chuo MUHAS wakishangilia baada ya kutunikiwa stashahada, shahada ya kwanza, shahada za uzamili, digrii za ubobezi na digrii ya uzamivu.

…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. David Homeli Mwakyusa, amewatunuku wahitimu 1,362 wa ngazi mbalimbali za masomo ya afya na sayansi shirikishi, zikiwemo stashahada, shahada ya kwanza, shahada za uzamili, digrii za ubobezi na digrii ya uzamivu jambo ambalo limeongeza mchango mpya katika kuimarisha sekta ya afya nchini.
Akizungumza leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya 19 ya MUHAS, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema kati ya wahitimu hao, 504 ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 37 ya jumla ya wahitimu wa mwaka huu.
Prof. Kamuhabwa ameeleza kuwa wahitimu 108 wamepata stashahada ya juu, 680 shahada ya kwanza, 511 shahada za uzamili, 54 digrii za ubobezi, na tisa wamehitimu digrii ya uzamivu ya udaktari wa falsafa.
Amefafanua kuwa MUHAS imeendelea kuwekeza kwenye TEHAMA ili kuboresha mazingira ya kujifunzia, kufundishia, kufanya utafiti na kuimarisha mifumo ya utawala.
Kwa mwaka 2025, chuo kimeboresha miundombinu na mifumo ya kidijitali, ikiwemo kufunga mifumo mipya ya serikali kama Government Service Directory (GSD) na mGov Platform kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Kuhusu utafiti, Prof. Kamuhabwa amesema chuo kimeratibu miradi 121 ya utafiti kwa mwaka wa masomo 2024/2025, hatua inayoonyesha ongezeko la ubunifu na mchango wa MUHAS katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, machapisho ya kitaaluma yameongezeka kutoka 324 hadi 577 kwa mwaka 2024/2025, huku bunifu 96 za wanachuo na wafanyakazi zikiendelea kuendelezwa ili ziweze kufikia soko kupitia ushirikiano na sekta ya viwanda na biashara.
Ameongeza kuwa MUHAS imezindua Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi (AHMMETF) unaolenga kusaidia tafiti, ubunifu na elimu ya afya kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema Baraza limeendelea kusimamia maendeleo ya chuo kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwajibikaji, usawa wa kijinsia na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa rasilimali.
Amesema pia kwamba chuo kimeanzisha mitaala mipya 14 ya shahada ya kwanza na za uzamili ili kukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya afya kitaifa na kimataifa.
Ameeleza kuwa programu 11 za uzamili na ubobezi zinalenga kuzalisha wataalamu bobezi watakaosaidia kuimarisha huduma za kibingwa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuunga mkono jitihada za serikali katika kuendeleza utalii tiba.
Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa MUHAS imeendelea kutoa ushauri kwa Serikali ya Tanzania katika maeneo mbalimbali, ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili, sera na miongozo ya huduma za afya ya mama na mtoto, pamoja na maboresho ya mitaala ya uuguzi ili kuongeza ubora wa wauguzi nchini.
Kwa upande wao, baadhi ya wahitimu akiwemo Jackline G. Malavanu na Alfred Chibwe, wameshukuru MUHAS kwa kuwapatia elimu bora na kuwajengea uwezo unaowawezesha kutekeleza majukumu yao kitaaluma na kwa ufanisi.



