Na. Meleka Kulwa- Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel Makubi, ametoa wito kwa Watanzania wenye matatizo ya masikio, Koo pamoja na mfumo wa pua kufika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na hospitali zingine nchini ili kuweza kupata matibabu.
Ametoa wito huo Desemba 4, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kambi ya mafunzo na matibabu ya upasuaji wa koo, sikio pamoja na mfumo wa pua kwa kushirikiana na Shirika la Hands-Giving Life (HGL) kutoka Uturuki lililoanzishwa mwaka 2020.
Aidha amebainisha kuwa kambi hiyo inajumuisha madaktari 10 kutoka Uturuki chini ya shirika la Hands-Giving Life (HGL)
Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa kambi hiyo ya matibabu ya upasuaji wa koo, sikio pamoja na mfumo wa pua ilianza tarehe 1 Desemba na yatatamatishwa Desemba 7, 2025.
Akizungumzia lengo la kambi hiyo, Prof. Makubi amesema kuwa lengo ni kutoa matibabu kwa wananchi, huku akibainisha kuwa watu 10 wenye changamoto ya masikio watafanyiwa upasuaji wa sikio. Aidha amebainisha kuwa walijitokeza watu 30 wenye uhitaji wa kufanyiwa upasuaji, lakini kambi hiyo ilipanga kuhudumia watu 10 kulingana na kuwa kwa siku wanafanyia upasuaji mtu mmoja hadi wawili.
Aidha, amesema kuwa kambi hizo zitakuwa endelevu kwa wagonjwa watakaokuwa na uhitaji wa kufanyiwa upasuaji, akibainisha kuwa upasuaji huo utakuwa ukifanyika kwa kushirikiana na hospital ya Taifa ya Muhumbili.
Kwa upande wake, Rais wa Shirika la Hands-Giving Life (HGL) Hatice Eller kutoka Uturuki amesema kuwa wamefurahishwa na nafasi ya kushirikiana na BMH kutokana na hospitali hiyo kuwa miongoni mwa hospitali bora nchini. Aidha, ameishukuru menejimenti ya BMH kwa ushirikiano mzuri tangu maandalizi hadi kuanza kwa huduma.
Aidha, mmoja wa madaktari Prof. Dr. Aysegiil Datiogly walioungana na msafara huo amesema kuwa mafunzo yatahusisha nadharia na vitendo ili kuwaongezea uwezo washiriki. Aidha, amebainisha kuwa matibabu yatatolewa zaidi kwa wagonjwa wenye changamoto za masikio, ingawa wengine pia watapata huduma kulingana na uhitaji.




