Wazee mkoani Dar es Salaam wamezungumza katika mahojiano maalum na Fullshangwe Media leo Desemba 02, 2025, huku wakisema wana matarajio makubwa na hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Leo Rais Dkt. Samia anazungumza na wazee na kuhutubia taifa katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Bi. Zainabu, mkazi wa Kigamboni, amesema eneo lao bado linakabiliwa na changamoto kubwa ya barabara kutokuwa katika hali nzuri, hali ambayo imekuwa kikwazo kwa wananchi. Aidha, amebainisha kuwa vijana wa Kigamboni na maeneo ya Kimbiji wanakabiliwa na changamoto ya ajira huku wengi wakizurura mitaani licha ya kuwepo kwa viwanda vinavyoajiri zaidi watu waliohamishwa kutoka maeneo mengine, hivyo ameshauri iwepo mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.
Amesema changamoto za mikopo kwa akina mama bado ni kubwa licha ya kuahidiwa mikopo isiyo na riba.
Aidha, Bi. Zainabu amesema wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025 eneo lao lilikuwa na amani na utulivu na kwamba wananchi waliwahi kushirikiana na viongozi kusimamia utulivu wakati wa uchaguzi na waliwaeleza vijana madhara ya kushiriki katika vitendo vya vurugu na vijana waliwasikiliza kulikuwa na utulivu.
Kwa upande wake, Kilimba Lyanga, Ally Kessy, mkazi wa Dar es Salaam, amesema uzalendo wa vijana umepungua ikilinganishwa na kipindi chao cha ujana, ambapo kulikuwa na taasisi nyingi zilizojenga uzalendo ikiwemo mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria. Amesema ukosefu wa ajira ni sababu kubwa ya vijana wengi kuhangaika mitaani licha ya kumaliza vyuo na shule.
Ameongeza kuwa baadhi ya viongozi wanapotoa kauli zinazotafsiriwa vibaya na wananchi, zinachangia kupunguza matumaini ya vijana kuhusu mustakabali wa taifa. Aidha, amebainisha kuwa Watanzania ni waelewa na wanaweza kuelewa kwa haraka endapo viongozi watatoa kauli za kuonyesha mifano mizuri tofauti na kauli zinazoweza kuwakatisha tamaa wananchi.




