Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles D.Kihampa (wa tatu kutoka kushoto),akisoma uamuzi wa Tume kusitisha kibali cha udahili na usajili kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), leo jijini Mwanza, baada ya Chuo Kikuu cha Mwanza, kudahili na kusajili idadi kubwa ya wanafunzi wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu, mwaka wa kwanza wa masomo 20225/26.
………
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesitisha rasmi kibali cha udahili na usajili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu katika Chuo Kikuu cha Mwanza (MzU) kwa mwaka wa masomo 2025/2026, kufuatia ukiukwaji mkubwa wa taratibu za udahili.
Hatua hiyo imetangazwa jijini Mwanza, leo na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles D. Kihampa, ambaye amesema uamuzi huo unatokana na ukaguzi wa awali uliofanywa na Tume baada ya kukamilika kwa zoezi la udahili nchini kote.
Profesa Kihampa amefafanua kuwa kati ya Julai 15 hadi Oktoba 20, 2025, TCU iliratibu maombi ya udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/26, huku vyuo vikipewa mamlaka ya kuendelea na udahili kwa kuzingatia sheria na taratibu za kitaaluma.
Hata hivyo, katika ukaguzi uliofanywa na Tume, imebainika kuwa Chuo Kikuu cha Mwanza kimedahili wanafunzi wa Udaktari wa Binadamu mara kumi zaidi ya idadi iliyoidhinishwa na TCU jambo ambalo limezidi uwezo wa chuo katika miundombinu, vifaa na rasilimali watu, hasa walimu.
Profesa Kihampa alisema kuwa, katika kikao chake maalum cha 127 kilichofanyika Novemba 28, 2025, TCU ilifikia maamuzi makuu manne:Kusitisha kibali cha udahili wa mwaka wa kwanza kwa Shahada ya Udaktari wa Binadamu katika MzU kwa mwaka wa masomo 2025/26.
Pia,chuo kilishindwa kurekebisha idadi ya wanafunzi licha ya maelekezo ya Tume, hivyo kuendelea kukiuka taratibu za kitaaluma ambapo Tume imeruhusu wanafunzi waliokwisha sajiliwa na kuripoti chuoni hapo, kuhamia vyuo vingine, vinavyoidhinishwa kudahili kozi hiyo au vinginevyo, kwa mwaka huu au miaka ijayo.
Aidha, imeundwa Kamati ya Wataalamu kuchunguza mifumo ya kitaaluma ya chuo ili kuhakikisha kinazingatia sheria na kanuni za uendeshaji wa elimu ya juu.
Licha ya kusitishwa kwa udahili wa mwaka wa kwanza, wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu katika MzU wataendelea na masomo kama kawaida.
Profesa Kihampa amewahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa mchakato wa uhamisho utasimamiwa kwa weledi na kasi, kwa kushirikiana na vyuo vitakavyowapokea wanafunzi huku akieleza kuwa TCU inalinda maslahi ya wanafunzi na jamii, na ndiyo sababu hatua hiyo imechukuliwa kuhakikisha viwango vya elimu vinadumishwa.
MzU pia imeelekezwa kutoa taarifa kwa wanafunzi kuwa hakitatoa masomo kwa mwaka 2025/26 na kinatakiwa kuwasaidia kwa ukaribu katika kupata uhamisho.
Katibu Mtendaji huyo alisisitiza kuwa TCU itaendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia na kuthibiti ubora wa elimu ya chuo kikuu nchini, pamoja na kuhakikisha viwango vya elimu vinakidhi matarajio ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
“Tutahakikisha vyuo vikuu nchini vinafuata sheria, kanuni na miongozo yote ya uendeshaji wa elimu ya juu,” alisema Profesa Kihampa.



