Na John Walter-Babati
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mhe. Daniel Sillo, ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Manyara kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya Dareda Kati – Dareda Misheni yenye urefu wa kilomita 7 ili ikamilike ndani ya muda uliopangwa na kuanza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Sillo ametoa wito huo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake tayari umeanza rasmi na umefikia asilimia 5%.
Amesema kuwa baada ya kukamilika kwa uchaguzi, sasa ameanza kazi ya kuwatumikia wananchi na kufuatilia utekelezaji wa miradi yote muhimu katika jimbo lake.
Ameihakikishia TANROADS na wananchi kuwa serikali itaendelea kutoa fedha za ujenzi kwa wakati, ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Manyara, Mhandisi Dutu Masele, amesema kuwa wamejipanga kikamilifu kusimamia mradi huo na kwamba timu yao ipo eneo la ujenzi kila siku.
Amesisitiza kuwa hata wakati huu wa msimu wa mvua, kazi zitaendelea bila kukwamishwa na changamoto za hali ya hewa.
Amesema changamoto kubwa kwa wananchi hakuna, na kilichobaki ni kukamilishwa kwa taratibu za fidia ili baadhi yao wapate nafasi ya kupisha eneo la mradi kama inavyotakiwa.
Wananchi wa eneo hilo wameipokea kwa matumaini makubwa kasi ya ujenzi, kwani barabara hiyo wameisubiria kwa muda mrefu kutokana na umuhimu wake katika kuwaunganisha wakazi wa wilaya za Babati na Mbulu, sambamba na kurahisisha usafirishaji wa mazao yao ya biashara kama vitunguu swaumu, vitunguu maji, viazi na mazao mengine.
Barabara hiyo ni sehemu ya mradi mpana wa ujenzi wa barabara ya Dareda – Dongobesh yenye urefu wa kilomita 60, unaofadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania.
Kazi ya ujenzi inatekelezwa na Kampuni ya Jiangxi Geo Engineering Group Corporation kutoka China.
Mkataba wa ujenzi ulisainiwa Aprili 6, 2024, ingawa mkandarasi alichelewa kuanza kazi kutokana na changamoto mbalimbali za awali.
Mpaka sasa mkandarasi huyo tayari amelipwa malipo ya awali shilingi 1,482,348,968.60, sawa na asilimia 15 ya gharama za mradi.
Wananchi wamesema wana imani kuwa utekelezaji wake utakapokamilika, barabara hiyo itafungua fursa zaidi za uchumi na kuimaris
ha maisha yao kwa ujumla.





