Na Meleka Kulwa, Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, ameanza rasmi ujenzi wa zahanati katika Mtaa wa Maseya, Kata ya Hombolo Makulu, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ulioshirikisha mamia ya wananchi, Mavunde aliwashukuru wananchi wa Maseya kwa imani waliyoionyesha kwake, kwa Diwani wao na kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kura nyingi walizopata kwenye uchaguzi huo.
“Nawashukuru wananchi wa Maseya kwa kumchagua Rais Samia, mimi na Diwani wetu kwa kura nyingi sana. Kazi yetu sasa ni kutatua changamoto za wananchi, na leo tumeanza ujenzi wa zahanati yetu ambayo italeta huduma za afya karibu zaidi na wananchi,” alisema Mavunde.
Mbunge huyo aliahidi kuchangia matofali 2,000 na mifuko 100 ya saruji ili kufanikisha ujenzi wa jengo hilo hadi hatua ya upauaji. Aidha, aliongeza kuwa ana imani serikali itashirikiana nao katika kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Maseya, Alexander Fwalu, aliishukuru serikali ya Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo hilo, ikiwemo usambazaji wa umeme na uchimbaji wa visima vya umwagiliaji kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, miradi ambayo imesaidia wakulima kupata maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo.
Fwalu pia alimpongeza Mbunge Mavunde kwa hatua ya haraka ya kuanza ujenzi wa zahanati hiyo, akiahidi kuwa wananchi wa Maseya watatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na huduma za afya zinapatikana karibu na wananchi.




