Kagera
Miradi 8 ya barabara za lami zenye urefu wa KM. 5.2 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 zimepitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru katika halmashauri 8 mkoani Kagera.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Kagera Mhandisi Wilson Charles amesema kuwa barabara za lami zilizopitiwa na mwenge wa uhuru ni miongoni mwa kilometa 8 zilizokamilika kwa mwaka 2023/2024.
Amesema miradi hiyo imeweza kuwaondolea adha za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa halmashauri hizo kwani barabara hizo zimejengwa maeneo ya kutolea huduma za kijamii ikiwemo shule,zahanati,vituo vya afya,hospitali,viwandani pamoja na kwenye makazi ya watu.
“Barabara hizi zimekuwa na maana sana katika kuboresha huduma kwa wananchi ambapo awali hakukuwa na barabara na hivyo kusababisha wananchi kushindwa kupita na kupata huduma za kijamii kwa wakati kwa sababu ya barabara”.
“Barabara za lami zimeongeza mabadiliko makubwa sana katika swala la kuongeza hadhi na kukuza miji na vijiji ,tunasimamia vizuri wakandarasi na vijiji vinaendelea kupata lami,wananchi wanapata taa za barabarani na kukuza uchumi wao na sisi hatutachoka tutaendelea kutekeleza kwa weledi mkubwa sana”ameongeza Wilson
Mkoa wa Kagera una mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TARURA zenye urefu wa kilometa 6,403 na kati ya hizo kilometa 132.2 tayari zina Lami na mwaka 2024/2025 TARURA imepanga kujenga barabara ya lami KM. 8.