Na Sophia Kingimali
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini Zambia lengo likiwa kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo huku akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kumbukumbu ya miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo na kulihutubia Bunge la Zambia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Oktoba 21, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema ziara hiyo ya Rais Dk. Samia ni ya kwanza kitaifa nchini humo baada ya ziara ya kiserikali kuhudhuria uapisho wa Rais wa nchi hiyo, Hakainde Hichilema alipochaguliwa mwaka 2021.
“Sisi Tanzania na Zambia tunao ushirikiano wa muda mrefu wa kihistoria na malengo makuu ya ziara hiyo ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo hasa katika maeneo ya kimkakati ambayo ni uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu,” amesema Makamba.
Pia, kujadiliana namna bora ya kushirikiana kuboresha uendeshaji wa miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kama bomba la mafuta la TAZAMA, Reli ya Tazara na kukubaliana namna ya kuweka mazingira wezeshi na kirafiki kwa wafanyabiashara na wasafirishaji kufanya shughuli zao kwa urahisi.
Makamba amesema ziara hiyo itaibua fursa mpya za ushirikiano kwa nchi hizo na kuongeza chachu ya maendeleo na pia Rais Dk. Samia kufanya mazungumzo na Rais Hichilema, Jumuiya ya Wafanyabiashara ya nchi hiyo kuhusiana na maboresho makubwa yanayofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Bandari yetu ya Dar es Salaam ni muundombinu unaohitaji soko na kama ujuavyo bandari zinashindana na nyingine katika ukanda huu, ili iendelee kuwa chachu ya uchumi lazima ipate soko na mzigo na ukitazama moja ya soko lake kubwa ni mzigo wa Zambia,” alisema.
Amesema takribani asilimia 80 ya mzigo wote unaoingia Bandari ya Dar es Salaam na kwenda nje ya nchi unapitia katika mpaka wa Zambia kwenda Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Pia Rais Dk. Samia amealikwa kuhudhuria kongamano la biashara na uwekezaji ambalo litashirikisha wafanyabiashara wa nchi hizo huku wanaotoka Tanzania wakiwa 100.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia amepata heshima ya huhutubia bunge la Zambia ambapo juzi bunge hilo limetoa azimio la kutengeneza kanuni ya kuwezesha Rais kulihutubia.
Aidha,Waziri Makamba amesema Tanzania inatarajia kusaini mikataba na hati za makubaliano mbalimbali ambazo zitaleta tija na kuimarisha ushirikiano, ulinzi, sayansi na teknolojia, biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo.