Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida leo tarehe 07 Septemba, 2023 amehutubia Kongamano la Uwekezaji nchini China lililoandaliwa na Baraza la Umoja wa Mamlaka za Kuhamasisha Uwekezaji za Majimbo ya China (CCIIP).
Katika hotuba yake, Dkt. Kida amebainisha mikakati ya Serikali ya Tanzania kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.
Aidha, Dkt Kida ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha Wawekezaji wa China kuwekeza nchini na kutumia fursa za uwekezaji na masoko za ndani na ukanda wa SADC.
Nchi ya China ni miongoni mwa vyanzo vikubwa cha mitaji kutoka nje (FDI) ndani ya Tanzania ambapo tangu mwaka 2013 wakati wa ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya watu wa China takribani mtaji wa dola za Marekani bilioni 10 zimewekezwa nchini.
Katibu Mkuu Dkt. Kida anaendelea na ziara ya kikazi nchini China, ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki katika Ufunguzi wa Maonesho ya Biashara na Uwekezaji yanayofanyika jiji la Xiamen, Jimbo la Fujan, China.




