Na Sophia Kingimali
SERIKALI imesema suala la uchanjaji wa Mifugo bado lipo chini nchini hivyo imepanga kushirikiana na Sekta binafsi kufanya kampeni ya Chanjo nchi nzima.
Hayo ameyasema Leo Septemba 6 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulenga Jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa pembeni wa jukwaa la mifumo ya chakula Afrika AGRF uliowakutanisha mawaziri wa uvuvi na mifugo na wadau katika sekta hiyo wenye lengo la kuelezea fursa zinazopatika nchini katika sekta ya hiyo.
“Hatua hiyo itasaidia kuipa Tanzania uwezo wa kusomeka katika ramani duniani kuwa inauwezo wa kupambana na Magonjwa hasa yanayoonekana kuwa na uwezo wa kuambukiza hata binadamu”amesema Ulega
Aidha akizungumzia kuhusu malisho amefafanua kuwa Wizara ya Mifugo, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha zote kwa pamoja zimeonyesha utayari wa serikali katika kuhakikisha suala la upatikanaji wa malisho ya uhakika ili ng’ombe wasiendelee kufa kwa ukame.
Ameongeza kuwa hata wazalishaji wa kuku wakati wa kiangazi wanapata wakati mgumu wa malisho kwa kuwa mahindi huwa yanapanda bei sana na hivyo yanaongeza gharama ya uzalishaji.
Amesema wamezungumza kwa pamoja na wadau ikiwa ni pamoja na kuwapati Ardhi ili wafanyekazi ya uzalishaji.
Waziri Ulega, amesema wao kama wasaidizi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan , wameonyesha utayari wa kuhakikisha wanatatua changamoto zinazoikabili sekta ya uzalishaji nchini hasa kwa kuyaleta pamoja makundi ya vijana na kina mama katika uzalishaji.
Kwa upande wake mwekezaji sekta ya Mifugo Mariam Sekuwe amesema akiwa mfugaji anayemiliki ng’ombe zaidi ya 100 na mmiliki wa kiwanda cha kusindika maziwa wanayo furaha kuona jukwaa la AGRF linakuwa fursa katika kupanua wigo wa uwezeshaji wa sekta ya mifugo na masoko lakini changamoto ni malisho kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo ni vyema wataalamu kutumia jukwaa hilo kujadili namna ya kukabiliana na athari zilizopo.
Amesema, amehamasika kupitia jukwaa hilo kuongeza uzalishaji na kufikia soko la Afrika katika mifumo ya chakula na kusisitiza haja ya wizara kutumia nafasi hiyo kuwawezesha wafugaji kwa kuwapatia dawa, maabara za kisasa za mifugo na wataalamu ili kukabiliana na kupe ambao ni tishio kwa ng’ombe wengi nchini.
Nae mwanzilishi wa mradi wa malisho ya wanyama ambae ni mnufaika wa BBT Rogasian Njau amesema kufuatia juhudi zinazofanywa na serikali wamepatiwa eneo la hekari 250 Kwa ajili ya kufanya kilimo Cha malisho ya wanyama.
“Tunamshukuru sana mama Samia kwa kutusaidia vijana hasa katika sekta ya mifugo Kwani tunasaidia katika mnyororo wa thamani katika sekta ya mifugo ili mifugo iweze kupata chakula cha kutosha bila kujali hali ya hewa ndio maana sisi tunafanya kilimo cha malisho ya mifugo na kuhakikisha chakula cha mifugo hakikosekani Mmuda wote.”amesema Njau



