Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde (katikati), akizungumza na Wanafunzi wa Sekondari ya Mwanzi iliyopo Manyoni mkoani hapa wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua ujenzi wa shule kupitia mradi wa BOOST aliyoianza jana Julai 9, 2023.

………………………………………………

Na Dotto Mwaibale, Singida

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI
(ELIMU) Dk. Charles Msonde amezihimiza Halmashauri za Wilaya kote nchini
kukamilisha miradi ya ujenzi wa shule zinazojengwa kwa fedha za BOOST ili
Tanzania iwe nchi ya mfano kwa mataifa mengine kuja kujifunza mafanikio ya
sekta ya elimu kutokana na kukamilika kwa miradi hiyo kwa kiwango cha juu.

Dk. Msonde ameyasema hayo leo Julai 9, 2023
wakati alipotembelea miradi ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari za
Halmashauri za wilaya za Manyoni, Itigi, Ikungi na Singida.

Msonde alisema Halmashauri zihakikishe
zinakamilisha miradi ya BOOST ifikapo Julai 30, 2023 ili wanafunzi wajiunge
katika shule na kuanza kutumia majengo hayo.

‘Tanzania itakuwa nchi ya mfano katika uboreshaji
wa miundombinu ya shule na nina amini kwa nchi nyingine za Afrika na mataifa
mengine yatakuja kujifunza kuona jinsi tulivyofanikiwa kutokana na kazi kubwa
na nzuri aliyoifanya Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi
kwenye sekta ya elimu,” alisema Dk.Msonde.

Alisema fedha zilizopokelewa kwa awamu ya
kwanza  ambazo zimetolewa kama mkopo na
Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kutekeleza mradi huo  wa BOOST kwa miaka mitano ni  Sh. Trilioni 1.15 na umelenga kuimarisha
ujifunzaji katika elimu ya awali na msingi.

Dk.Msonde alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la
wanafunzi wanao maliza kidato cha nne kwenda cha tano na sita hivyo kwa kuwa
Serikali ni sikivu ikaona ni vema kujenga shule hizo kwa ajili ya wanafunzi
hao.

Katika ziara hiyo Dk.Msonde alizipongeza
halmashauri za Manyoni, Ikungi na Singida kwa kuzisimamia vizuri fedha hizo na
kutekeleza miradi hiyo kwa viwango na kwa wakati na akahimiza kuongeza kasi
zaidi iliikamilike ndani ya muda uliopangwa.

“Nawaombeni ongezeni kasi ya kukamilisha
mradi huu kwa kuweka mafundi wengi ambao watakuwa wakishambulia kila kona
badala ya kusubiri mafundi waliopo kufanya kazi hiyo peke yao huku kasi yao
ikiwa ndogo,” aliongeza Msonde.

Baadhi ya shule alizotembelea na kukagua ujenzi
huo ni Shule ya Sekondari ya Mwanzi iliyopo Manyoni, Shule mpya ya Msingi ya
Igonoa iliyopo Itigi, Shule ya Sekondari ya Mwanamwema Shein ambayo ipo Kata ya
Mgori Wilaya ya Singida na Shule ya Msingi Minyaa iliyopo Kata ya Kinyeto
Wilaya ya Singida.

Kesho Dk.Msonde atamalizia ziara yake mkoani hapa
kwa kukagua ujenzi wa shule hizo katika Wilaya ya Mkalama na Iramba na
kuzungumza na watumishi wa sekta ya elimu na kufanya majumuhisho ya ziara hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde, akipanda mti wa kumbukumbu katika viwanja vya Shule Mpya ya Msingi ya Ikungi B wakati wa ziara hiyo.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde, akikagua ujenzi wa Bweni katika Shule ya Sekondari ya Ikungi. Kushoto ni Mkuu wa Shule hiyo, Neema Stephano na kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, DK. Elpidius Baganda, akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwanzi wakati Dk.Msonde alipofika kukagua ujenzi wa madarasa na mabweni unaoendelea katika shule hiyo.
Diwani wa Kata ya Mgori, katika Halmaashauri ya Wilaya ya Singida, Mnyangoi Zuma, akiishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha za ujenzi wa shule mpya ya kidato cha tano na sita.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde, akisisitiza jambo wakati akizungumza na walimu na wananchi alipokuwa akikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mwanzi wilayani Manyoni.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde. akisalimiana na Diwani wa Kata ya Manyoni, Saimon Mapunda.
Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Manyoni, Adelini Mwanisi, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo.
Ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Mwanzi ukiendelea. Kulia ni Afisa Elimu Mkoa wa Singida, DK. Elpidius Baganda,
Ukaguzi wa ujenzi wa mabweni hayo ukiendelea.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde, akitoka kukagua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi, Igonoa iliyopo Itigi.
Walimu wa Hamashauri ya Wilaya ya Ikungi wakipongezwa kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde, akimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwa kazi nzuri inayofanywa na halmashauri hiyo chini ya uongozi wake.
Muonekano wa ujenzi wa madarasa yanayojengwa Shule ya Sekondari ya Mwanamwema Shein yaliyopo Kata ya Mgori.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi  ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI (ELIMU) Dk. Charles Msonde, akimpongeza Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwanamwema Shein, Justina Chinemata kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia ujenzi wa shule hiyo.
Muonekano wa madarasa yanayojengwa Shule mpya ya Msingi ya Minyaa iliyopo Kata ya Kinyeto Wilaya ya Singida.