Jeshi la Paolisi Mkoa wa Mwanza linapenda kutoa taarifa ya kupatikana kwa mwili  wa askofu mstaafu wa kanisa la Aglikana Diocese ya Victoria Nyanza, Boniphace  William@Kwangu, Miaka 61, Mkazi wa Shibula, wilayani Ilemela, aliyekutwa  amefariki na mwili wake ukielea ndani ya maji kando ya ziwa victoria karibu na  eneo linapojengwa daraja la Dr. John Pombe Magufuli (JPM). 

Ni kwamba, tarehe 28.11.2022 majira ya asubuhi huko Shibula Wilaya ya Ilemela  Boniphace William@Kwangu aliaga familia yake na kuelekea wilaya ya  Sengerema kwa ajili ya kupokea malipo ya mwisho ya shilingi 2,500,000/= baada  ya kuwa ameuza eneo lake pamoja na nyumba kwa kanisa la KKKT- Sengerema.  Hata hivyo hakuweza kulipwa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa wanunuzi  walimtaka awasilishe nyaraka ya umiliki wa eneo hilo hivyo, alirudi Mwanza mjini  kwa ajili ya kushughulikia nyaraka hizo. 

Kwamba, ilipofika jioni ya siku hiyo familia yake walipata wasiwasi kuhusu alipo Boniphace William@Kwangu kwani hakuwa amerudi nyumbani pia alikuwa  hapatikani kwenye simu yake ya mkononi. Kutokana na hali hiyo ilibidi familia  yake watoe taarifa Kituo cha Polisi Kirumba. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na familia na watu mbalimbali  lilianza kufanya ufuatiliaji ili kubaini alipo askofu huyo mstaafu. Wakati  uchunguzi ukiendelea tarehe 01.12.2022 majira ya 10:00 jioni zilipatikana taarifa  kutoka kwa wananchi wema kwamba, huko katika kijiji cha Kigongo, kata ya  Idetemya wilaya ya Misungwi ndani ya maji katika ziwa victoria jirani na daraja la Dr. John Pombe Magufuli umeonekena mwili wa mtu wa jinsia ya kiume ukiwa  unaelea majini. Baada ya askari kwa kushirikiana na wananchi kuopoa mwili huo  ulitambulika kuwa ni wa Boniphace William@Kwangu.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali kwa hatua za kiuchunguzi kabla ya kukabidhiwa  kwa ndugu kwa ajili ya mazishi. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo  hivyo tunaiomba familia, ndugu, jamaa na wananchi kwa ujumla wenye taarifa  zozote kuhusiana na tukio hili wazitoe kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kufanyiwa  kazi. 

Imetolewa na:- 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza 

S.L.P 120, 

Mwanza.