Home Mchanganyiko MAKAMU WA RAIS AWATAKA WATANZANIA KUTUNZA FUKWE

MAKAMU WA RAIS AWATAKA WATANZANIA KUTUNZA FUKWE

0

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Philip Mpango akizungumza kwenye jukwaa la maendeleo endelevu linalofayika Jijini Mwanza

**********************

Na Hellen Mtereko,
Mwanza

Watanzania wametakiwa kuhakikisha wananusuru fukwe zilizopo nchini ili ziwe endelevu hatua itakayosaidia wafanyabiashara,wadau na sekta binafsi kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika fukwe kwa kutoa huduma pamoja na ajira.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatano Novemba 23 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango wakati akifungua jukwaa la maendeleo endelevu (GGP),lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi ili kujadili usimamizi madhubuti wa fukwe kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini linalofanyika kwa siku mbili ( Novemba23-24,2022) jijini Mwanza.

Dkt.Mpango ameeleza kuwa Tanzania imebarikiwa na Mungu kwa kuzungukwa na maji maeneo ya nchi na kuwa na fukwe za kuvutia kwa baadhi ya mikoa.

“Bado hatujaweza kutumia kikamilifu fukwe hizi kwa ajili ya maendeleo kama ilivyo katika nchi nyingine asilimia kubwa za fukwe zetu hazijaendelezwa zinakabiliwa na tatizo la uharibifu wa mazingira unaotokana na ongezeko la shughuli za binadamu kandokando ya fukwe ikiwemo uchimbaji wa mchanga, utupaji taka ovyo ikiwemo taka maji na taka ngumu ,ujenzi holela ,uvuvi haramu kilimo na ufugaji holela,”ameeleza Dkt Mpango.

Ameeleza kuwa athari hizo zinaonekana zaidi kando kando ya mito na kwenye fukwe za maziwa makubwa ikiwemo ziwa Victoria aidha mmomonyoko wa undogo kando ya fukwe umeripotiwa kuongezeka siku hadi siku katika mikoa ya Dar- es-salaam,Mtwara ,Tanga ,Lindi , Mwanza,Pwani na Visiwa vya Zanzibar.

Kwa upandewake Ofisa Mtendaji Mkuu kutoka Taasisi ya UONGOZI Kadari Singo,ameeleza kuwa jukwaa hilo ni la nane kufanyika tangu lilipo zinduliwa na ni moja ya programu kuu za Taasisi ya UONGOZI katika masuala ya maendeleo endelevu.

Lengo la Jukwaa hilo ni kukuza uelewa wa masuala ya uchumi wa kijani na mchango wake katika maendeleo nchini na linawakilisha zana ya kimaendeleo ya kujenga miunganisho ya kisekta, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kutunza mifumo ya ikolojia na mazingira.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameeleza kuwa serikali itaendelea kutunza fukwe ili zitumike kama sehemu ya utalii.

Akizungumza kwenye Jukwaa hilo Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratias Ndejembi, ameeleza kuwa Taasisi ya Uongozi itaendelea kutoa mafunzo na elimu mbalimbali kwa wananchi na viongozi ili kuhakikisha fukwe na mazingira yanatunzwa.