Gari la mizigo likipita kwenye moja ya daraja lililopo katika barabara ya Likuyufusi-Mkenda Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma.

Mojawapo ya daraja katika barabara kuu ya Likuyufusi-Mkenda inayotarajia kujengwa kwa kiwango cha lami na Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni.

Sehemu ya Barabara kuu ya Likuyufusi-Mkenda wilayani Songea  kama inavyoonekana,hata hivyo wananchi wa vijiji vinavyopitiwa na Barabara hiyo wameiomba Serikali kujenga kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Mrakibu wa Uhamiaji kituo  cha Mkenda wilayani Songea Upendo Kikudo  wa kwanza kushoto akiwaongoza baadhi ya watumishi wa idara na taasisi za Serikali kukagua daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.

Mrakibu wa Uhamiaji kituo cha Mkenda wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Upendo Kikudo wa pili kulia,akiwaeleza jambo Waandishi wa Habari Emmanuel Msigwa wa ITV na Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Ruvuma Endrew Chatwanga wa kwanza kulia, walioko kwenye kazi  kutembelea na kuandika habari za ujenzi wa miradi ya Barabara zinazotarajia  na zinazoendelea kujengwa na Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS)mkoa wa Ruvuma.

 Na Muhidin Amri,Songea

………………………………

WANANCHI wa vijiji  vinavyopitiwa na Barabara ya Likuyufusi –Mkenda na nchi jirani ya Msumbuji kwa upande wa mkoa wa Ruvuma,wameiomba Serikali kuanza ujenzi wa barabara  hiyo kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za usafiri wa abiria na mizigo hususani katika kipindi cha masika.

Wametoa  ombi hilo kwa nyakati tofauti  mbele ya waandishi wa Habari wa mkoa wa Ruvuma walioko kwenye ziara  ya kutembelea miradi  ya barabara inayotarajia  kutekelezwa na inayotekelezwa na Serikali  ya awamu ya sita kupitia wakala wa barabara Tanzania(TANROADS) katika mkoa wa Ruvuma.

Shaban Kilomoni mkazi wa kijiji cha Nakawale wilayani Songea alisema,katika  wilaya hiyo kuna fursa nyingi ikiwamo makaa ya mawe,hata hivyo  bado hayajaanza kuchimbwa wala kunufaisha serikali kutokana na tatizo  kubwa la miundombinu ya barabara.

Alisema licha ya rasilimali nyingi zinazopatikana wilayani humo,wawekezaji na wafanyabiashara wameshindwa kufika kutokana na ubovu wa barabara hiyo,jambo linalochelewa  sana maendeleo yao.

“kukosekana kwa barabara ya lami ni chanzo cha kusua sua kwa maendeleo  kwenye maeneo yetu,hali hii imechangia sana hata usafiri  kwenda Songea mjini huwa ngumu siyo wakati wa masika tu bali hata  muda wa kiangazi, na madereva wanatumia nafasi hiyo kupandisha  nauli kutoka Sh.3000 hadi 7000”alisema.

Kandedus Mbawala dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Songea mjini na Mkenda darajani alieleza kuwa,wakati wa masika wanalazimika kutumia kati ya masaa 3 hadi 4 kufika Songea mjini  na kama ingejengwa kwa lami muda huo ungepungua hadi  saa 1.

Alisema kuwa,iwapo Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami  basi itaharakisha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya,mkoa na nchi kwa ujumla.

Hata hivyo, ameipongeza TANROADS kujenga barabara hiyo kwa  changarawe,hali iliyo rahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji  kuendelea japo kwa shida wakati huu ambao serikali iko kwenye maandalizi ya kujenga kwa  kiwango cha lami.

Mrakibu wa Uhamiaji wa kituo cha Mkenda  Upendo Kikudo,alisema, watumishi wa serikali ni sehemu ya waathirika wakubwa  wa ubovu wa barabara hiyo kwani  wanapohitaji kwenda makao makuu ya wilaya na mkoa kikazi, wanalazimika kutumia muda mrefu na hivyo kuathiri shughuli za kuwahudumia wananchi.

Aidha,ameishukuru Serikali kwa kuonyesha nia ya kutaka kujenga barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu na  nchi jirani ya Msumbiji.

Kwa mujibu wa Kikudo,barabara hiyo ni muhimu  na kama itajengwa kwa lami itatumika kikamilifu  kusafirisha bidhaa kutoka Bandari ya Mtwara kwenda nchi jirani ya Msumbuji kwa kutumia kituo cha  forodha cha Mkenda.

Alisema, kwa sasa wafanyabiashara wengi wa Msumbiji wanalazimika kutumia bandari ya Dar es slaam na  hatimaye kupita mpaka wa Tunduma mkoani Songwe unaounganisha Zambia na Tanzania,badala ya Bandari ya Mtwara na mpaka wa Mkenda na kwenda moja kwa moja nchini Msumbuji,hivyo kuwaongezea gharama kubwa.

Aliongeza kuwa, serikali itakapojenga barabara ya lami kutoka Likuyufusi hadi Mkenda km 124,kuna uwezekano mkubwa hata wa kujengwa  kituo  cha pamoja (One Stop Border Post)ambacho kitawezesha taasisi zote za serikali kuwa sehemu moja na kuwasiliana kwa haraka.

Kofi Binasi  raia wa Msumbuji,ameziomba Serikali za nchi hizo  kuunganisha nguvu na kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuharakisha uchumi na maendeleo ya watu wa nchi hizo.

Kwa upande wake Meneja wa wakala wa Barabara
Tanzania(TANROADS)mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi alisema,Serikali iko mbioni kuanza ujenzi wa barabara  hiyo kwa kiwango cha lami na hadi sasa kazi iliyofanyika  ni upembuzi yakinifu.

Mlavi alisema kuwa,kwa sasa wako katika hatua za manunuzi kabla ya kumpata mkandarasi ambaye atajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kumaliza kabisa changamoto ya usafiri  na kufungua uchumi wa mkoa wa Ruvuma.

Alisema Serikali kwa kutambua umuhimu wa eneo hilo kiuchumi, katika awamu ya kwanza itaanza  kujenga km 60 za kutoka Likuyufusi hadi Muhukuru na baadaye itaendelea kujenga km 64 hadi Daraja la Mkenda linalounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.