Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na Operesheni, Misako na Doria katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01.04.2022 hadi tarehe 03.04.2022 jumla ya watuhumiwa 16 wamekamatwa kwa tuhuma ya makosa mbalimbali yakiwemo mauaji na kuingia nchini bila kibali [Wahamiaji Haramu] kama ifuatavyo:-
KUPATIKANA NA BHANGI.
Mnamo tarehe 01.04.2022 majira ya saa 23:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Inyara, Kata ya Iyunga, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa EMMANUEL ANDREW [48] Mkazi wa Inyara akiwa na bhangi kete 16 sawa na gramu 08. Mtuhumiwa ni mtumiaji wa dawa hizo za kulevya.
KUPATIKANA NA BIDHAA ZILIPIGWA MARUFUKU KUINGIZWA NCHINI.
Mnamo tarehe 01.04.2022 majira ya saa 21:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Nonde, Kata ya Mabatini, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya na kumkamata mtuhumiwa HAMIS MWAILUBI [40] Mkazi wa Nonde akiwa na chupa 16 za pombe kali aina ya Fiter, Ice Dry London Gin na Win ambazo zimepigwa marufuku kuingizwa nchini zikitokea nchi jirani ya Malawi.
KUSAFIRISHA BHANGI.
Mnamo tarehe 02.04.2022 majira ya saa 16:00 jioni huko katika kizuizi cha Polisi Chalangwa kilichopo Kata ya Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa katika kizuizi hicho walimkamata SALUM KARIBU [30] Dereva wa Gari yenye namba za usajili T.206 DPP aina ya Mitsubishi fuso, Mkazi wa Makongolosi akiwa anasafirisha bhangi kete 132 zenye uzito wa gramu 800 akiwa ameifunga kwenye box na kuweka ndani ya mfuko wa sulphate kama mzigo wa kawaida. Mtuhumiwa ni muuzaji wa dawa hizo za kulevya.
KUPATIKANA NA BHANGI.
Mnamo tarehe 02.04.2022 majira ya saa 12:30 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko maeneo ya Mshikamano, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya na Mkoa wa Mbeya na kumkamata ANDREW ESSABITORY [25] Mkazi wa ZZK Mbalizi akiwa na bhangi yenye uzito wa gramu 400 kwenye mfuko wake wa suruali. Chanzo ni kujipatia fedha kwa njia isiyo kuwa halali kwa kuuza kete 02 za bhangi kwa Tshs. 500/=.
KUINGIA NCHINI BILA KIBALI.
Mnamo tarehe 03.04.2022 majira ya saa 02:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kijiji cha Simike, Kata ya Utengule, Tarafa ya Ilongo, Wilaya na Mkoa wa Mbeya na Askari hao wakiwa katika msako walifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu kumi na moja [11] wote wanaume raia wa nchini Ethiopia ambao walipakiwa kwenye Gari yenye namba za usajili mbili T.497 ARB na nyuma ilikuwa namba T. 494 AEB aina ya Toyota Mark II rangi nyeupe.
Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kumsaka dereva wa Gari hiyo ambaye ndiye mwenyeji na aliyekuwa akiwasafirisha wahamiaji hao ambaye alitoroka na kulitelekeza Gari mara baada ya kuwaona askari Polisi. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa za mtu au watu wanaowatilia mashaka katika maeneo yao ili upelelezi na taratibu za kuwakamata ziweze kufanyika.
ATIWA MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke RIZIKI HENRY [22] Mkazi wa Nditu Wilaya ya Rungwe kwa tuhuma za mauaji ya mume wake aitwaye AYUBU ARON [33] Mkazi wa Nditu.
Ni kwamba mnamo tarehe 02.04.2022 majira ya saa 05:00 alfajiri huko Nditu, Kata ya Suma, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya AYUBU ARON [33] Mkazi wa Nditu alijeruhiwa kwa kupigwa na kitu butu kichwani na kuchomwa kitu chenye kali kisogoni na mke wake aitwaye RIZIKI HENRY [22] Mkazi wa Nditu.
Baada ya tukio hilo, mhanga alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana kwa matibabu lakini mnamo tarehe 02.04.2022 majira ya saa 17:30 jioni alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu Hospitalini hapo.
Chanzo cha tukio ni ugomvi uliotokana na mwanamke ambaye ni mtuhumiwa kuchelewa kurudi nyumbani na alipoulizwa ndipo ulizuka ugomvi uliopelekea kifo cha mwanaume. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana kwa uchunguzi wa kitabibu. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.